Bukobawadau

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:VIFO VYA MAHUJAJI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kufariki kwa Mahujaji zaidi ya 700 na wengine zaidi ya 800 kujeruhiwa wakati wakishiriki ibada ya Hijja iliyofanyika Makkah, Saudi Arabia tarehe 24 Septemba, 2015.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania, Saudi Arabia
Mahujaji hao walifariki na kujeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea kwenye eneo la Mina.

Aidha, taarifa hizo zinaeleza kuwa hadi sasa Mahujaji wapatao watano (5) kutoka Tanzania wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa. Majina ya Watanzania waliofariki na kutambuliwa ni Bi. Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla. Mtu mwingine aliyefariki ni Raia wa Kenya anayeishi nchini ambaye ametambulika kwa jina la Bi. Fatuma Mohammed Jama.
Ubalozi unaendelea na jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine aliyefariki kwenye tukio hilo. Aidha, Serikali ya Saudia imetangaza kuwa itatoa taarifa kamili ikiwemo idadi ya watu waliofariki na majeruhi na nchi wanazotoka mara itakapokamilika.
Pia Ubalozi wetu kwa kushirikiana na Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Hijja za Tanzania ikiwemo BAKWATA pamoja na Mamlaka za Serikali ya Saudi Arabia unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo kuna vifo na majeruhi wengine kutoka Tanzania.
Hivyo basi, Wananchi wanaombwa kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
25 Septemba, 2015
Next Post Previous Post
Bukobawadau