Bukobawadau

YALIYOJIRI MDAHALO WA MKIKIMKIKI LEO

Leo Jumapili Septemba 27, 2015 tunawaletea midahalo ya Mkikimkiki na leo utajikita kwenye uchumi, wawakilishi wa vyama kwa leo ni;

1. Onesmo Kyauke ambae ni mshauri wa ilani UKAWA
2. Khamis Kigwangalla akiwakilisha Chama Cha Mapinduzi
3. Hamimu Honga akiwakilisha ACT wazalendo
4. Eugine Kabendera akiwakilisha CHAUMA
5. Jacob Samuel akiwakilisha ADC
Mdahalo wa Mkikimkiki Uchumi na usawa 27 sept 2015

Swali la utangulizi; Kwa mwananchi wa kawaida unapozungumzia uchumi unarejea bei za bidhaa na huduma, mfumuko wa bei ni asilimia 9.1 (Benki ya Dunia). Nini Sera ya Chama chako kuelekea Uchaguzi Mkuu?

Dr; Honga (ACT - Wazalendo): Kipato cha Mtanzania wa kawaida kimeendelea kuwa kile kile, mfumuko wa bei humuathiri mkulima kwani mazao hubakia bei ile ile licha ya mfumuko mkubwa wa bidhaa zingine.

Serikali imekuwa ikiwakopa wakulima na kuwalipa baadae kwa fedha ya awali, bila kujali mabadiliko kwenye soko. Kipato kinachopatikana hakinmufaishi mkulima huyu.

ACT itaweka bima ya mfumuko wa bei na bima ya mazao/mifugo ili kumhakikishia mkulima endapo kutakuwa na mfumuko.

Mfumo wa hifadhi ya jamii utahakikisha kila mwananchi anakuwa na kinga!

Jaco Joel Samweli (ADC): Mfumuko wa Bei hutokea pale mfumo wa fedha na uchumi unapoharibika. Hutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi au upungufu wa bidhaa kwenye soko, kupungua kwa maingizo na matoleo ya bidhaa... (Demand and Supply).

Kukiwa hakuna udhibiti wa fedha, sarafu kupoteza thamani yake huchangia pia mfumuko wa bei.

ADC inaamini katika Ujamaa wa Kidemokrasia, huu utaendana na mfumo wake wa kiuchumi ambapo wananchi, taasisi zao na dola hushirikishwa kwa pamoja kwenye uchumi. Kwenye ilani yetu tumesema tutarekebisha mifumo yote inayotawala, hasa mfumo wa biashara ya ndani.

Mfumo huu utalinda sarafu yetu na utamlinda mlaji, mtumiaji wa bidhaa. Serikali itasimamia soko!

Hamisi Kigwangala (CCM): Ilani ya CCM imejikita kwenye uchumi na usawa, hii ndio roho ya maisha ya watu ya kila siku. Tutakaposhika dola, Serikali ya Ndugu Magufuli itasimamia kukuza uchumi kwenye maeneo manne; uzalishaji, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wananchi, kujenga uchumi wa viwanda vitakavyotumia malighafi za ndani, ujenzi wa miundombinu na huduma zingine za kiuchumi.

Tunalenga kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wadogo na kufunga mianya ya ukwepeji wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa.

Eugene Kabendera (CHAUMMA); Katika ILANI yetu kuna mambo kadhaa kuhusu uchumi; Nchi yetu ina gesi asilia, hatua kadhaa zimeshafanyika kutumia gesi kwenye umeme. Nishati bado ni kikwazo katika uzalishaji, serikali ya CHAUMMA itawekeza gesi iliyopo katika nishati ili kuanzisha viwanda vingi zaidi kadiri ya uzalishaji.

Tutauza bidhaa nje badala ya mazao; mfano; kuuza unga wa mahindi badala ya mahindi ghafi.

Onesmo Kyauke (UKAWA); Mfumuko wa bei unaendana na kushuka kwa thamani ya sarafu. Kikubwa ni kuongeza uzalishaji, UKAWA wataunganisha sekta zote za uchumi.

UKAWA itawekeza kwenye elimu na utafiti ili kupata wataalamu wa kiwango cha juu na cha kati. Hii ndio namna pekee ya kukuza sekta mbalimbali za uchumi (kilimo, ufugaji na uvuvi). Kuimarika kwa sekta hizi kutakuza pia viwanda vidogo vya usindikaji, hivi vitamilikiwa na wananchi wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika.

Serikali ya UKAWA itaimarisha miundombinu ili kuvutia wawekezaji wa kimataifa! Miundombinu ya reli, barabara na kadhalika...

Kuimarika kwa miundombinu kutaimarisha pia sekta ya UTALII. UKAWA wamejipanga kufufua sekta za usafirishaji wa anga ili kuvutia watalii wengi hivyo kukuza uchumi.

Sekta ya Uwekezaji itasimamiwa kuhakikisha inabakisha fedha ndani ya nchi.
============================== =========

Swali la Pili (Eyakuze) kwa Jacob Joel; Ukuaji wa uchumi umechangiwa na vitu vitatu; misaada na ruzuku, uwekezaji wa kigeni na mikopo ya nje, ambapo deni la taifa limeongezeka. Tanzania ni taifa tegemezi kwa kiasi kikubwa, ni vyanzo gani mbadala vinavyopendekezwa na chama chako?

Jacob: Mfumo wa ADC ni Uchumi Shirikishi, kwa sasa dola ndiyo hudhibiti uchumi. Mwalimu Nyerere wa enzi za Ujamaa alisema Uhuru ni kazi, si jambo la mchezo.

ADC ikingia madarakani itapunguza uombaji wa misaada nje, kukopa na kuachia uchumi kwa wawekezaji. Uchumi wetu utashikiliwa na wananchi wenyewe wakifanya kazi katika kile sekta na kukuza pato lao wenyewe.

Hamisi Kigwangala; Tutapunguza matumizi ya Serikali, kupunguza idadi na nguvukazi isiyo ya lazima kwenye wizara na wakala wa Serikali. Pato litakalopatikana litafanya mambo ya msingi.

Tutapunguza misamaha ya kodi kwa wawekezaji wakubwa, tutaongeza uzalishaji kwenye kila sekta na kupunguza kodi kwenye zana za kilimo.

Eugene Kabendera: Kuacha kutegemea wahisani sio ndoto, lazima kuwe na mkakati madhubuti wa Serikali. Ukweli ni kuwa itachukua muda hadi kufikia kujitegemea kamili. Kwa kutumia gesi, Tanzania tutakuwa wazalishaji kuliko waagizaji, hivyo kuongeza fedha za kigeni nchini.

Onesmo Kyauke: Kutegemea sana wageni ni kuweka nchi rehani, UKAWA itakuza uchumi kwa asilimia kumi na kuendelea kila mwaka. Tutafanya hivi kwa kuimarisha kilimo kulingana na mahitaji nje ya nchi...

Kilimo huzaa viwanda, tutakuwa na viwanda vya kuongeza thamani!

Walipo madarakani kwa miaka 54 watueleze wamefanya nini.

Hamisi Hongo; Tegemezi litaisha tukichaguliwa kwa kuwa tutapunguza misamaha ya kodi na kufunga mianya yote ya ukwepaji kodi.

Serikali yetu itakuwa na mawazirri 15 pekee, hivyo kubana matumizi.

Tutajenga uchumi shirikishi, kila mwenye uezo wa kufanya kazi atawezeshwa afanya kazi vizuri na achangie pato la taifa. Tunao mpango wa kuongeza pato la taifa kwa asilimia 25.

Tutawashughulikia wezi, kurudisha nidhamu!
==============================
Swali kutoka kwa mchangiaji, Pazi Kauzeni; Mtawezaje kurejesha viwanda vilivyotelekezwa? Wenzetu Zambia wana kampuni ya kusafisha mafuta ghafi, sisi chetu, TIPER tumekiua!

Hamisi Kigwangala; Serikali haiwezi kujenga viwanda, sera hizo zilikufa mwaka 90 baada ya nchi kuingia kwenye soko huria. Serikali itaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji... Itavichukua viwanda vyote vilivyotelekezwa na kuwapa watu wengine wanaoweza kuviendeleza.

Kabendera: Tatizo ni watu ambao hawana utaalamu wa kuendesha viwanda hivyo, CHAUMMA imeliona hilo na litafanyiwa kazi. Bakhressa ameagiza wataalamu wengi kutoka nje, sisi pia tutafanya hivyo! Tunaweza kusamehe kodi, lakini kutakuwa na maelekezo ya kuviendesha, hasa katika ajira!

Kyauke: Ni upotofu kusema serikali haiwezi kumiliki viwanda, zipo nchi kubwa ambazo Serikali zake zinamiliki viwanda na mashirika. Nchi hii ilikuwa ya viwanda, Chama cha Mapinduzi kilibinafsisha vyote.

UKAWA itarudisha viwanda vilivyouzwa na kuimarisha mfumo wa elimu ya ufundi ili kutoa wataalamu wa kwene viwanda vidogo. Tutajenga mazingira rafiki kwa wawekezaji, kuboresha sekta ya nishati na kuimarisha upatikanaji wa wataalamu. Tutaimarisha soko la viwanda vitakavyoanzishwa.

Hamimu Hongo; ACT ina utaratibu wa kufufua viwanda vyote vilivyouwawa. Kwanza tutawashughulikia waliouziana viwanda kiholela. Tutakaribisha wawekezaji na tutawafuatilia watumie malighafi za humu nchini.

Serikali itamiliki viwanda mama, viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa ajili ya viwanda vingine. Tutaboresha masoko ya bidhaa za viwanda hivyo nje ya nchi! Wawekezaji watapewa kwa masharti maalumu.

Jacob Samuel; Kazi ya kujenga viwanda ni kazi ya wafanyabiashara, Serikali haijengi viwanda.. Serikali itajenga miundombinu.

Serikali itajenga mtandao mpana wa biashara za ndani, mfumo mpana wa biashara ili kutengeneza mfumo mzuri na mkubwa wa usambazaji wa bidhaa ndani ya nchi hivyo kuweka hali ya kutegemeana kiuchumi kati ya maeneo mbalimbali.

============================== ======
Shabani Shabani: Vyama vya siasa havijajikita katika kuimarisha sekta ya kilimo, sekta muhimu katika uchumi wa nchi.

Kabendera: Wakulima wote watupatie kura CHAUMMA ili tufanye yafuatayo;-

Bado wakulima wetu wanalima kwa jembe la mkono, tutaimarisha teknolojia ya kilimo na mikopo ya pembejeo za kilimo. Mikopo itatolewa kwa riba nafuu...

Onesmo Kyauke: Ilani ya UKAWA imezingatia sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji, bila kuimarisha sekta hizi huwezi kupambana na umasikini.

Kilimo kitakuwa cha kisasa, tutapambana kuondoa kabisa jembe la mkono. Tutaimarisha teknolojia ya uzalishaji ili kulima kwa tija kwa eneo dogo...

Tutakuwa na mazao mbadala, mfano kilimo cha miembe!


Wakulima hawatazuiwa kuuza mazao popote wanapotaka.

Dr. Hongo; Sera yetu ACT ni kuhakikisha mkulima anaboresha kilimo chake, fedha zitapelekwa kwenye hifadhi ya jamii kwa malengo ya kuboresha miundombinu ya kilimo na kutoa elimu kwa wakulima.

Serikali yetu haitamkopa mkulima hata siku moja, ufuatiliaji wa mazao, uzalishaji na akiba ya chakula utafanyika mapema kabisa. Wafanyabiashara wa mazao watakopeshwa kwa riba nafuu ili wakanunue kwa fedha taslimu na bei halali.

Jacob Joel: Mfumo wa kibepari huwapa kilimo wakulima wakubwa. Mfumo wetu wa kijamaa utawaunganisha pamoja wakulima wadogo-wadogo ili wawe na maeneo makubwa na walime pamoja.

Katika biashara zingine tutatazama aina ya biashara za kujikimu wanazofanya watu wa chini, tutabadili biashara zao kuwa kubwa.

Hamisi Kigwangala; Chama cha Mapinduzi kitasimamia Kilimo cha Biashara, kwa kuongeza uzalishaji, kupanua masoko na kuunganisha kilimo na viwanda vya kuongeza thamani bila kusahau miundombinu ya usafirishaji. HAdi sasa CCM imeboresha barabara kwa kiasi kikubwa hivyo kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka vijijini.

Wakulima watawezeshwa ili kuboresha kilimo chao, watapewa mikopo na kuwezeshwa kuanzisha viwanda vidogo.
============================== =========
Rashidi Swalehe Mrope; Ujamaa ni kama ulifeli. Mfumo wa Ubepari umekuwa ukishabikiwa kwa muda mrefu, mtu binafsi huweza kumiliki mali za umma. Mfumo huu umeweka tofauti kubwa za kipato. Ni mfumo gani mbadala?

Onesmo Kyauke: Ujamaa haukuwa mfumo mbaya kwa maana yake, soko huria haliwi soko holela! Serikali ya UKAWA itavutia wawekezaji wenye mitaji ya kigeni, kuwezesha wawekezaji wa ndani na kuwasimamia wawekezaji hawa.

Tutatoza kodi kwa wawekezaji hawa. Huduma za jamii zitaboreshwa, UKAWA itatoa elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.

Dk. Hongo; Tutajumlisha ujamaa, demokrasia na Unyerere. Kila anayeweza kufanya kazi atafanya kazi na atalipwa kadiri ya kazi yake. Hakuna mtu atakayenyanyaswa kwa utajiri wake, bali atawajibika kwa mujibu wa sheria.. Kulipa malipo stahiki kwa wafanyakazi na kulipa kodi!

Jacob Joel: Chama cha Mapinduzi na ACT ni vyama vya kikomunisti, ADC ni chama cha Ujamaa wa Kidemokrasia, mfumo huu unasimama katikati ya Ujamaa na Demokrasia.

Socalist Market economy iliasiliwa na China, CCM pia walijaribu kufanya mabadiliko kwenye Ujamaa, wakaja na Azimio la Zanzibar, wakauza kila kitu cha umma. ADC itawapa wananchi maamuzi juu ya rasilimali zao.

Kigwangala: Mambo ya mifumo yanawachanganya watu wengi, CCM ni chama cha kijamaa ambacho kimeamua kufanya mageuzi ndani na ujamaa, kuingiza vionjo vya kibepari kama soko huria na ushindani wa uchumi.

Eugene Kabendera: Hatuwezi kuwa tofauti na nchi zinazotuzunguka, kubadili mfumo mazima kuna athari kubwa kwa uchumi. CHAUMMA itasimamia, ila sio kudhibiti uzalishaji. Kila mtu atatakiwa kutekeleza wajibu wake kwenye uchumi!

Mahakama itawezeshwa kusimamia kesi, maamuzi mengi ya mahakama yameumiza uchumi wa nchi. Bunge litasimamiwa pia...

==============================
Dan Nkuru kutoka Marekani: Tanzania imejipa matumaini makubwa ya kuuza gesi, wanasiasa wameitumia kama turufu ya kampeni. Zao la kwanza litatoka mwaka 2020, makubaliano ya Iran kuhusu nyuklia yatashusha bei ya gesi, vipi kama tutakosa mapato tunayotarajia, kuna mpango gani wa kuifanya gesi iwe kwa matumizi ya nyumbani na kulinda mazingira?

Hamimu Hongo; Gesi itawezesha kupata umeme wa bei nafuu, viwanda vitapunguza gharama za uzalishaji hivyo kushusha bei ya bidhaa sokoni.

Gesi itawezesha uzalishaji wa mbolea, kushuka kwa bei ya mbolea kutaleta tija kwenye kilimo.

Miti inakatwa kwa kutengeneza mkaa na kuni za kupikia, upatikaji wa gesi utarekebisha hai hii. Hata tusipopata soko la nje, yapo mambo ambayo gesi itatufaa.

Jacob Joel: ADC tunaamini kwamba umeme wa gesi hautakuwa hauwezi kuwa nafuu zaidi ya maji. Mchakato wa kuifanya gesi izalishe umeme ni wa gharama kubwa. Tumeimba sana wimbo wa dhahabu na sasa yamebaki mashimo, wimbo wa gesi unaweza kutupeleka huko.

ADC haina matarajio makubwa kwenye gesi, ila marekebisho ya kimfumo!

Kigwangala: Tusipokuwa makini, rasilimali huweza kuleta maafa badala ya faida. Tumetunga sera na sheria ambazo zitahakikisha rasilimali ya gesi inawanufaisha Watanzania.

Tunatengeneza Sera ya Kuwanufaisha Wazawa, sera hii itawabana wachimbaji kuwafaidisha wazawa, mwekezaji atanunua bidhaa zake za kila siku miongoni mwa wananchi.

Joel: Kupitia gesi, Mtanzania atafaidika endapo bei ya umeme itapungua. ADC itashusha bei ya umeme utakaozalishwa na gesi, tutaendelea kuusambaza hadi maeneo ya mbali. Hiyo ndiyo namna Mtanzania atanufaika.

Kyauke: Neema ya gesi itanufaisha nchi, ila tunahitaji kiongozi imara. Mgombea wa UKAWA amesema mara nyingi kuwa atasimamia hilo. Bunge la kwanza litafuta Sheria ya MAfuta na Gesi ambayo ilipitishwa kinyemela na Serikali.

Tutatumia gesi kuzalisha umeme, ili kukuza sekta za viwanda na biashara. Tutabadili matumizi ya nishati ili kuepusha nchi kuwa jangwa, dalili ambazo zimeshaanza kuonekana kutokana na uvunaji wa mkaa na kuni.

============================== ========
Maswali kuhusu Ajira na vijana, Masunga Selemani; Kwanini taasisi nyingi za mikopo hazina masharti rafiki kwa vijana?

Jacob: Ajira hutolewa katika sekta kubwa tatu; sekta ya umma (serikali, wakala na taasisi zake), sekta binafsi (biashara na wafanyabiashara) na sekta ya uchumi wa kijamii.

Aliyejiajiri huingia kwenye mikopo anapopungukiwa na mtaji, ADC itatengeneza sheria zitakazosiamia maslahi ya pande zote mbili.

Kigwangala: CCM ina mikakati mingi katika kutatua tatizo la ajira. Serikali itatenga maeneo ya halmashauri, asilimia 30 ya tenda za halmashauri zitapelewa kwa vikundi vya vijana watoa huduma na wanaoishi kwenye maeneo husika.

Mikopo ya bei nafuu kutoka benki ya Ujasiriamali.

Asilimia 5 ya mapato ya halamashauri itaenda kwa vijana na asilimia tano nyingi nne ikaenda kwa akina mama.

Eugene Kabendera: CHAUMMA italegeza masharti ya mikopo kutoka kwenye halmashauri, mikopo hii huenda kwa waajiriwa badala ya vijana wa kawaida. Benki zitasimamiwa na Sera elekezi itakayotungwa na Serikali ili zitoe mikopo kwa vijana na kwa masharti nafuu.

Kyauke: Vijana wengi hawakopesheki kwa kuwa hawana dhamana, ni hatari kuwakopesha. Makundi madogo yatakuwa na benki zake kwa ajili ya kuwawezesha wadau wa makundi hayo.

Tutaanza na kuelimisha kabla ya kukopesha, tutatoa elimu kwa haya makundi kwanza ili kuhakikisha mikopo inaleta faida kwao.

Benki maalumu itaundwa kwa ajili ya kukopesha vijana.

Hamimu Hongo; Serikali itahakikisha mabenki hayamilikiwi na watu wa nje, tutarudisha umiliki wa mabenki kwa wananchi. Tutatumia hifadhi ya jamii kuwekeza kwenya ajira za vijana kwa kuwakopesha na kuasisi viwanda.

============================== =======
Jafari Ndege; Je, watakabiliana vipi na mtikisiko wa kuporomoka kwa shilingi? Matumizi ya Dola humu nchini yanavutia ukuaji wa dola...

Kigwangala; Kushuka kwa shilingi ni matokeo ya uchumi unaotegemea kuagiza kila kitu kutoka nje, Serikali itawekeza kwenye viwanda, kuzuia au kupunguza uagizaji kutaimarisha shilingi yetu.

Hairuhusiwi kutumia fedha nyingine kwa matumizi ya ndani, kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kukosa uwajibikaji. Serikali ijayo itaheshimu na kusimamia Sheria zilizowekwa.

Kabendera: Wanaocheza na dola ni wafanyabiashara wakubwa, Mtanzania wa kawaida hajawahi hata kuiona hiyo dola, licha ya kuwa waathirika wakubwa wa kupanda kwa dola. Kuongeza uzalishaji ndio muarobaini wa kushuka kwa fedha yetu, CHAUMMA tutatekeleza hayo kwa vitendo.

Kyauke; Si wakati wote thamani ikishuka ina madhara hasi, China inapigana kuweka thamani chini ili kuchochea mauzo ya bidhaa zao. Sisi hatuzalishi ndio maana tunaathirika!

UKAWA itafufua viwanda na kuongeza uzalishaji na tutahakikisha fedha za kigeni hazitumiki kwa uholela hapa nchini...

Dk Hongo: Wanaovunja sheria za fedha ni wakubwa, ndio maana hawachukuliwi hatua. Kuuza kwa wingi ndio suluhu ya kushuka kwa fedha yetu, kama hali itaendelea hivi tutaagiza hado unga wa dona.

Jacob Joel: Thamani inashuka kwa kuwa imekaa muda mrefu ikidorora hivyo kusababisha mfumuko mkubwa sokoni.

Mwaka jana tulishuka thamani kwa sababu ya ESCROW, kwa kuwa wafadhili walizuia fedha za kigni kuingia kwenye uchumi wetu, hivyo kushusha upungufu wa fedha za kigeni.
============================== ============
*****MUDA UMEONGEZWA****
============================== ============
Iddi Ngaluma: Ukuaji wa teknolojia umepunguza ajira, tunawezaje kukuza uchumi kwenye mazingira haya? Nini kifanyike kukuza uchumi huku tukiendana na teknolojia.

Kabendera: CHAUMMA kinakubali kabisa mabadiliko chanya ya kiteknolojia, Tanzania bado hatujawa waathirika kwa teknolojia viwandani kwani hata hivyo viwanda havipo. Serikali ya ADC itashadadia teknolojia na kuiwekea sera ili isiathiri ajira zetu.

Kyauke; Ni kweli teknolojia inaathiri ajira, Serikali ya UKAWA haitaogopa teknolojia, tutasimamia ubunifu wa vijana ili waweze kujiajiri.

Tukiboresha elimu tutazalisha vijana amabo watazalisha ajira badala ya kuwa wategemezi wa kuajiriwa! Wataalamu waliopo watatumika kwa ufanisi zaidi, kutakuwa na mgawanyo mzuri wa utaalamu!

Dk. Hongo; Tunaunga mkono ukuaji wa teknolojia. Mfumo mbovu wa Serikali ndio unafanya teknolojia kuwa adui, nguvukazi ambayo imekosa kazi kutokana na teknolojia itawezeshwa kufanya mambo mbadala badala ya kuwa walalamikaji.

Serikali ya ACT imeweka mpango maalumu kupitia vipaumbele vyake vikuu vinne, hasa uchumi shirikishi.

Jacob Joel; ADC itasimamia dhana faafu za kiuchumi. Kadiri tutakavyosimamia kukua kwa teknolojia, ndivyo tutaweza kuboresha jamii zetu. Teknolojia inawezesha zaidi kuliko kubomoa kama tutakuwa makini!

Serikali ya ADC itafanya rasilimali watu kuwa mitaji watu, kwa kuwawezesha kwa maarifa na ujuzi, itaboresha vyuo vya ufundi stadi kama mbinu ya kufanya mageuzi haya.

Kigwangala; Kadiri tunavyoenda, tunapunguza zaidi matumizi ya misuli na badala yake tunatumia akili. Tunatarajia Mtanzania atumie zana, akili na maarifa mapya kuboresha maisha, teknolojia ni baraka zaidi. Wapo vijana ambao wameajiriwa na kujiajiri kupitia teknolojia, mfano; Max Malipo.

============================== ========
Cholo Fundi: Ni ipi dhana ya kukua kwa uchumi, ni kukua kwa pato ghafi la taifa au kukua kwa maisha ya wananchi?

Onesmo Kyauke, UKAWA; Kukua kwa uchumi lazima kuonekane kwenye maisha ya watu, kukua kwa pato ghafi kunaweza kusiakisi maisha ya mtu mmoja mmoja.

Serikali ya UKAWA itaambana na umasikini na kuboresha maisha ya Watanzania. Ni dhana potofu kuanza kupambana na watu binafsi kwa kusababisha matatizo ya kiuchumi, matatizo ni ya kimfumo...

Tanzania inahitaji mtu mwenye maono, UKAWA tunaye huyo kiongozi! Sera zetu zimejieleza vizuri kwenye kuboresha maisha ya wananchi!

Hamimu Hongo, ACT - Wazalendo; Maana halisi ya kukua kwa uchumi ni uwezo wa mtu mmoja mmoja kuweza kupata huduma za kijamii bila rabsha. Kukua kwa uchumi kitakwimu hakuna maana yoyote, kunamaanisha kunufaika kwa wezi na watawala wachache.
CREDIT JF
Next Post Previous Post
Bukobawadau