Bukobawadau

NENO LA SHUKRANI KWA WADAU WA “SIASA ZA BUKOBA”



Ndugu Wadau,
 Ni miezi mitatu sasa toka kuanzishwa kwa Jukwaa la “SIASA ZA BUKOBA” kupitia Mtandao wa Whatsapp. Tulipoanzisha Jukwaa hili, nia ilikuwa ni kuendeleza dhima ya Bukoba Wadau Media kwa kuwapa fursa wanaKagera hususani wanaBukoba walioko nje ya mkoa na nje ya nchi waweze kujua nini kinaendelea kwenye siasa za uchaguzi mkuu kwenye majimbo ya Bukoba. Tunaamini tumelitimiza vema jukumu hili na tumekidhi hitaji la wadau wetu kwa kuwawezesha kupata taarifa za papo kwa papo viganjani mwao. Ni imani yetu kwamba tumehabarisha juu ya mambo yaliyotendeka nyumbani bila ubaguzi wala upendeleo kwa mtu au chama chochote. Na iwapo katika kutenda kazi hii tulimkwaza mtu, tunaomba msamaha. Hakika haikuwa dhumuni wala kusudi letu.

Ili kufanikisha zoezi la ukusanyaji taarifa na habari mbalimbali tuliweka ada ya mwezi ya TZS 5,000 kwa kila mdau. Tunawashukuru wadau wote waliotuchangia. Na wale waliotuchangia zaidi ya kiwango  tunawashukuru kwa ukarimu wao. Tunaamini hata wale wote ambao bado hawajalipa ada zao, wataithamini kazi yetu kwa kufanya hivyo mara moja.

Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba uchaguzi umeisha na dalili zote zinaonyesha tumedumisha jadi yetu kwa kukamilisha zoezi hili salama, kwa umoja na amani. Sasa ni wakati wa viongozi wetu kutimiza ahadi zao. Bukoba Wadau Media tutaendeleza jukumu letu la kuwafikishia pongezi wakifanya vema, kuwakosoa wakifanya kinyume na kuwashauri watakapohitaji.

Kwenye Jukwaa letu katika nyakati tofauti tofauti kumekuwepo na mada zikihitaji muendelezo wa ajenda ya maendeleo kwa ajili ya Bukoba. Wako wadau waliofika mbali zaidi kwa kupendekeza ianzishwe Asasi ya Kiraia. Tunapongeza na kuungana na mawazo haya. Sisi kama Bukoba Wadau Media tunaahidi kuendeleza mchango wetu kwenye jitihada hizi kwa kuwaunganisha wadau wengi zaidi na kufikisha habari hizi kwa jamii ya ndani na nje ya mipaka yetu. Kulingana na majukumu na miiko ya tasnia yetu, tunapendekeza usukani wa jitihada hizi uratibiwe na watu binafsi wataopendekezwa na wadau badala ya kuratibiwa na Bukoba Wadau Media ambayo ni taasisi rasmi toka mwaka 2013.

Kumekuwa na mapendekezo ya kutaka viongozi wateule wa ngazi mbalimbali (Udiwani na Ubunge) katika manispaa ya Bukoba kuunganishwa kwenye Jukwaa hili. Tumelipokea wazo hili na kulifanyia kazi. Wako viongozi walioonyesha utayari wa kujiunga nasi. Lakini ili viongozi hawa waweze kushiriki kikamilifu katika mijadala, tunadhani ni tija zaidi kuwa wanaletwa kwa muda maalumu na kuondolewa baada ya mada au shughuli waliyoitiwa. Kwa sababu uzoefu umeonyesha kuwa, kuwemo katika Jukwaa si uthibitisho kwamba mwanachama anasoma au kupitia michango yote. Hivyo kuwa na uhakika, njia bora ni kuwaalika kwa mada maalumu na kisha kuwaondoa. Tunadhani kwa njia hii, wadau pia watakuwa huru zaidi kuwajadili viongozi wao.

Jukumu la kwanza la Jukwaa letu liliendeshwa chini ya jina “SIASA ZA BUKOBA” Sasa limekamilika tena kwa mafanikio makubwa. Tunapokwenda jukumu la pili tunapendekeza kubadili jina na kuwa “MAENDELEO YA BUKOBA” Hivyo kama hatutapata pingamizi ndani ya saa 24 tutabadili jina kuakisi jukumu jipya la Jukwaa letu.

Tunawashukuru sana wadau.

Imetolewa na Uongozi wa Bukoba Wadau Media
Next Post Previous Post
Bukobawadau