Bukobawadau

TAARIFA YA POLISI KUHUSU KIFO CHA MCHUNGAJI MTIKILA

Mnamo tarehe 04/10/2015 majira ya saa 05:45hrs huko Msolwa Kata ya Bwilingu barabara kuu ya Dar es Salaam –Morogoro, Wilaya ya Ki-Polisi Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Gari No. T.189 AGM aina ya Toyota Corolla likiendeshwa na George Steven Ponera miaka 31, mkazi wa Mbezi Mwisho Dar es Salaam liliacha barabara kisha kupinduka na kusababisha kifo cha Christopher Mtikila miaka 62,mpangwa, mchungaji wa Kanisa la Assemblies, na mwenyekiti wa Chama cha siasa DP mkazi wa Kinondoni “B” Dar Salaam.


Katika ajali hiyo, watu watatu waliokuwamo ndani ya gari hilo na marehemu Mchungaji Mtikila walijeruhiwa ambao ni Ally Mohamed miaka 42 mkazi wa Mbezi Dar es Salaam, yeye alipata maumivu shingo, mabegani na kifuani, mwengine ni Patrick Mgaya miaka 37 ambaye ni mchungaji
wa Kanisa la Assemblies of God mkazi wa Mbagala Dar es Salaam ambaye alikuwa na michubuko midogo usoni na kuumia kichwani, pamoja na George Steven miaka 31 mkazi wa Mbezi Dar es Salaam ambaye alipata michubuko kidogo eneo la mabegani. Majeruhi wote walipatiwa matibabu katika Kituo cha afya Chalinze na badae wawili kati yao katika Hospitali teule ya Tumbi na waliruhusiwa kutokana na hali zao kuendelea vizuri.

Baada ya kutokea kwa hiyo ajali, timu maalum ilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya ufuatiliaji wa ajali hiyo ikiongozwa na Mkuu wa utawala wa Traffic kuu Dar es Salaam SACP J. Kahatano, pamoja na mimi mwenyewe,Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Pwani na kuwashirikisha wataalamu wa Forensic Makao Makuu ya Polisi ACP Kashindye na Dokta A. Makata.
Uchunguzi wa mwili wa marehemu tayari umefanyika, na taarifa ya Daktari aliyefanya uchunguzi huo katika Hospitali ya Rufaa tumbi Kibaha jana tarehe 04/10/2015 umeonyesha kuwa, kifo cha marehemu kimesababishwa na kuvunjika kwa mbavu nane (8) upande wa kushoto na kuingia kwa damu kwenye mfumo wa hewa na kusababisha kushindwa kupumua.
 

Kabla ya ajali hiyo kutokea marehemu na wenzake tarehe 02/10/2015 jioni waliondoka Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Njombe na kufika tarehe 03/10/2015 alfajiri kwa ajili ya kampeni za Chama chao cha DP. Wakiwa huko walipata ajali kwa kugonga magari mawili yaliyopata ajali na
kusababisha uharibifu wa gari lao.Kulingana na taarifa ya Mkaguzi wa magari ya tarehe 03/10/2015 huko Njombe walishauriwa walitengeneze kwanza kabla ya kulitumia tena.Tarehe 03/10/2015 saa
21:30hrs waliondoka Njombe kwenda Dar es Salaam na ilipofika saa 05:45hrs katika eneo la Msolwa ndipo wakapata ajali hii.Uchunguzi uliofanywa kwa kukagua tukio na kuwahoji majeruhi walionusurika (katika eneo hilo hakuna watu wengine walioshuhudia tukio hilo kwa kuwa si eneo la makazi ya watu, ni mbuga). Ajali hii imeonyesha kuwa imesababishwa na sababu
Zifuatazo:
1. Mwendo kasi , dereva mwenyewe anakubali kwamba alikuwa mwendo kasi licha ya kuwepo kwa alama zinazooonyesha kwenda mwendo wa Km 50 kwa saa.
Aidha baada ya kuacha barabara kuu, gari hilo lilikwenda umbali wa mita 125 kabla ya kupinduka hali inayoashiria kuwa lilikuwa kwenye mwendo kasi.
2. Uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu kwa kuendesha gari mchana na usiku kucha kabla ya
kuanza safari walikuwa wakishughulikia matengenezo ya gari hilo ambapo hakupata muda wa kupumzika.
3. Kutofunga mkanda ya usalama . Katika uchunguzi inaonyesha marehemu hakufunga mkanda kwa kuwa alirushwa nje kupitia kioo cha mbele (wind screen).
4. Ubovu wa gari. Gari hilo lilipata ajali tarehe 03/10/2015 na moja ya sehemu muhimu iliyoharibika ni mfumo wa usukana (steering system) yawezekana halikupata matengenezo kikamilifu na hivyo kuchangia kutokea kwa ajali hiyo.
Hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kuwafichua maderva wanaokwenda mwendo kasi kupitia namba 08007575 ama 0715 009953 au 0658 376012. Aidha niwatake madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kwa wale watakao kaidi Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani hatutasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengi.  

 Asanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa PwaniKamishina
Msaidizi Jafari Ibrahim.
Next Post Previous Post
Bukobawadau