Bukobawadau

BI PASCHAZIA BARONGO ''NIMEREJEA KUSAIDIA KUINUA ELIMU NYUMBANI ''

Bi Paschazia Barongo pichani Mkurugenzi wa Chuo cha Ualimu ERA kilichopo Bukoa
Anaandika Phinias Bashaya,Mwananchi
Mapambano ya wanawake wenye malengo ya kuhakikisha ndoto zao zinatimia kwa kutumia fursa zilizopo yanakumbana na vikwazo vya kukatisha tamaa katikati ya mfumo unaoibua changamoto mpya kila siku.

Ndivyo ilivyo kwa Paschazia Barongo ambaye pengine ndiye mwanamke pekee nchini aliyefikia kiwango cha kufanikiwa kupambana na changamoto mbele yake kuanzisha chuo cha ualimu.
Safari yake haikuwa rahisi hadi kuwa na usajili wa chuo katika Kata ya Kitendagulo Manispaa ya Bukoba kwa ajili ya kufundisha walimu wa daraja la III A na kuwa alisimama imara kuhakikisha anaifikia ndoto yake ya baadaye ya kuwa na kituo cha elimu kinachoandaa vijana katika fani tofauti.
“Nilikutana na vikwazo vingi njiani hadi kufikia hatua hii lakini ‘I was too strong’, ningeweza kutumia fedha yangu kwenye mambo mengine, lakini nilijua Serikali pia inahitaji wadau katika elimu kama ilivyo kwenye sekta nyingine,’ anasema Paschazia
 Anasema chuo hicho kilichoanzishwa miaka miwili iliyopita kimelenga zaidi kutoa huduma kuliko kufanya biashara na kuwa anaamini ana uwezo wa kufanya jambo kubwa zaidi, huku akiwa na mtazamo wa kuwa na kituo cha elimu kitakachotoa kozi tofauti.
“Niliingia kwenye elimu lengo siyo kuwa na chuo cha ualimu, nataka baadaye iwe’Education Center’itakayofundisha fani nyingine pamoja na kuwaandaa vijana kwenye masomo ya kilimo biashara,’’anasema.
Kwamba kwa umri wake wa miaka 53 anaamini ana uzoefu uliomsukuma kutafakari na kuchukua hatua kwa vitendo na huo ndiyo mwanzo wa jina la chuo cha (ERA) ambao ni ufupisho wa ‘Experience, Reflection and Action’
Arejea nyumbani
Anasema alikuwa na sababu nyingi za kubaki nchini Sweden akifurahia maisha kama walivyo Watanzania wengine waishio nje ya nchi, lakini aliona ana deni la kurudi nyumbani kutoa mchango katika elimu.
“Nilikuwa na sababu nyingi za kutofikiria hata kurudi lakini suala la elimu liliniumiza hasa kwa wanafunzi ambao hawakuandaliwa katika mazingira mazuri kielimu ukilinganisha na wanaofundishwa shule binafsi kwa gharama,’’ anasema.
 Anasema suala la wazawa wa Mkoa wa Kagera kuwekeza katika maeneo mengine na kutelekeza nyumbani ni miongoni mwa mambo yanayoufanya mkoa kudumaa na kuporomoka kiuchumi. Hata alipofunga safari ya kurejea nyumbani na kuwekeza katika elimu bado aliowacha ughaibuni wanahoji sababu ya kuacha mazingira mazuri na maisha yasiyo na karaha na kujitumbukiza kwenye mfumo wa kutafutana.
‘’Kwa mazingira tuliyokuwa tunaishi, wengi wanaogopa kurudi wakilinganisha na changamoto zisizo za lazima watakazokuta huku nyumbani, mimi walinishangaa niliwaambia Tanzania ni nyumbani lazima niwekeze huko,’’anasema Paschazia.
 Hata hivyo, anasema Serikali na wadau wanatakiwa kujenga mazingira rafiki yatakayowavutia wazawa walioko ndani na nje ya nchi kuwekeza badala ya kuwekewa vikwazo vinavyokatisha tamaa.
Katika hatua hii ndipo anashangaa maajabu ya nchi hii kwamba ilikuwa lazima fomu zake zipitishwe na baraza la madiwani ili akubaliwe kuwa mmiliki utaratibu aliosema unasababisha usumbufu usiokuwa wa lazima.
“Sitaona vibaya kama Ofisa Elimu au jopo la wataalamu wa elimu litakuwa na jukumu la kukupitisha kuwa mmiliki, lakini sheria inawapa nguvu madiwani kusaini fomu ili ukubaliwe ni kikwazo na usumbufu,’’anasema.
Mwanamke huyo mwenye fani ya uuguzi anasema wengi wanakumbwa na woga katika masuala mbalimbali na wapo wanaokimbilia majukwaa ya siasa badala ya kusimamia na kuendeleza mambo mazuri waliyoanzisha. ‘’Mimi naamini mwanamke ana uwezo wa kufanya jambo kubwa kumzidi hata mwanaume jambo muhimu ni kupaza sauti yako na kujiamini kuwa unaweza ukiona umekwama kwenye plan A siyo kosa kwenda hata plan D,’’ anasema Paschazia na kuongeza kuwa:
“Wanawake wengine wanatafuta ‘status’ kupitia majukwaa ya siasa badala ya kupigania mafanikio kupitia masuala mengine ya maendeleo kwenye jamii, wapo wanaofanya mambo mengi, lakini hayajulikani kwa kuwa wamekimbilia kwenye siasa.’’
Anasema wapo wanawake wanaojulikana kwenye siasa, lakini hawajulikani kwenye mambo mengine makubwa waliyofanya kwenye jamii, wengine wamekumbwa na uoga unaowapunguzia kujiamini kufanya mambo makubwa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau