Bukobawadau

GARI LA ZIMAMOTO LAZINDULIWA WILAYANI KARAGWE NA ZAIDI YA MILIONI ISHIRINI ZACHANGWA KATIKA HARAMBEE ILI KULIBORESHA GARI HILO

Hatimaye baada ya matukio ya moto kuikumba Wilaya ya Karagwe mara kwa mara na kusababisha  hasara kubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo kutokana na kutokuwa na gari la Zimamoto uongozi  wa Wilaya hiyo kupitia Mkuu wa Wilaya Mhe. Deodatus Kinawilo ulifanikisha juhudi za kupata gari la kuzima moto wakati janga hilo linapotokea.

Gari hilo lilitolewa na Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto nchini na lilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu Juni 8, 2016 katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na kurikabidhi kwa Mkuu wa Kituo cha Wilaya cha Jeshi la Zimamoto na Uokozi Karagwe Sajenti P.F. Mmbale tayari kwa ajili kukabiliana na majanga ya moto.
Pamoja na gari hilo kutoka nchini Japani kuzinduliwa lakini kimuundo limetengenezwa kwa ajili ya kazi za uokoaji pamoja na kuzima moto maeneno ambayo yana vyanzo vya maji kama ‘fire hydrant’, visima vikubwa, mabwawa pamoja na sehemu ambazo gari kubwa za zimamoto hazifiki kwa hiyo kutokana na  mazingira ya Wilaya ya Karagwe kutokuwa miundombinu hiyo ya maji gari linahitaji kuboreshwa.
Maboresho hayo ni pamoja na kuwa na msaada wa kuwepo na gari linalobeba maji safi (water bowzer) pindi tukio la moto likitokea bowzer na gari la zimamoto yaongozane kutoa msaada wa maji wakati wa kuzima moto. Au gari la zimamoto lijengewa tanki la maji kulingana na uwezo wake angalau lita 2000 kwani  gari hilo lilikuwa halikutengenezwa kwa  lengo la kubeba maji bali ni (Movable Pump).
Baada ya Mkuu wa Mkoa kupokea taarifa na kuonekana kuwa gari hilo pamoja na kuzinduliwa lakini ili liweze kufanya kazi linahitaji kuboreshwa na kulikuwa kunahitajika kiasi cha shilingi milioni (20,000,000/=)  Mhe. Kijuu aliamua kuendesha harambee ambapo wadau mbalimbali na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwapamoja walichangia  katika harembee hiyo.
Katika harambee hiyo zilipatikana fedha taslimu 2,710,000/=, hundi shilingi 1,200,000/= , ahadi shilingi 10,850,000/=, kiwanja cha kujenga ofisi za Jeshi la Zimamoto chenye thamani ya shilingi 8,000,000/= na mabati yenye thamani ya shilingi 500,000/= kwaajili ya kujenga banda la kuhifadhia gari hilo, jumla ya thamani yote ni shilingi 23,260,000/=.
 Akiwashukuru wadau wote na watumishi waliochangia katika harambee hiyo Mhe. Kijuu alimshukuru pia Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Zimamoto nchini Jenerali Thobias Adengenye  kwa kuipa kipaumbele  Wilaya ya Karagwe kati ya magari 9 nchini wilaya hiyo pia nayo imepewa gari moja kutokanan na uhitaji mkubwa uliokuwepo.
Mkuu wa Mkoa pia aliwasistiza wananchi wa Wilaya ya Kargwe kuona umuhimu wa gari la zimamoto na kulifananisha na jeshi katika nchi yoyote wakati wa amani kwamba wananchi wanaweza kuona kama jeshi halina kazi na linatumia fedha za bure lakini vita ikitokea kwa siku moja huleta madhara makubwa sana kwa nchi kama moto unavyotokea na kusababisha hasara kubwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Deodatus Kinawilo alisema kuwa alimua kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Zimamoto  nchini (Jijini Dar es Salaam) kuomba gari la zimamoto baada ya kupata taarifa kuwa kulikuwa na magari tisa (9) yaliyokuwa yameletwa nchini baada ya wilaya yake kukumbwa na janga la moto katika mji mdogo wa Kayanya na kuunguza soko  kuu ambapo vibanda 117 viliungua na kuteketea mapema mwaka huu 2016.
Matukio makubwa ya moto yaliyowahi kuikumba Wilaya ya Karagwe tangu mwaka 2014 ni shule ya Sekondari ya St. Peter Clever bweni liliungua na kuteketea, mwaka 2015 Shule ya Sekondari Kayanga bweni la wavulana liliungua na kuteketea, mwaka 2016 vibanda 117 vya soko kuu la Kayanga viliteketea kwa moto pamoja na makanisa mawili kuchomwa moto.
Next Post Previous Post
Bukobawadau