Bukobawadau

MKUU WA MKOA AFANYA ZIARA KIWANDANI KAGERA SUKARI KUJIONEA UZALISHAJI NA AKIBA YA SUKARI ILIYOPO SASA

Kutokana na sakata la uhaba wa sukari nchini Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu aliamua kufanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha Kagera Sukari ili kujionea jinsi kiwanda hicho kinavyoendelea na uzalishaji, aidha kuona akiba ya sukari ilipo kwa sasa na kupata taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa sukari katika mkoa wa Kagera na mikoa ya jirani.
 Katika ziara hiyo iliyofanyika Juni 07, 2016 MKuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alipokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa sukari kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Bw. Ashin Rana ambapo taarifa yake ilijikita katika uzalishaji na usambazi wa sukari kwa mwaka 2015/2016 na mwaka huu 2016/2017 hasa katika kipindi cha Aprili, Mei na Juni 2016 ambapo kumekuwepo na uhaba wa sukari nchini.
Bw. Ashin Rana alisema kuwa kwa mwaka 2015/2016 kiwanda kilikuwa kinazalisha jumla ya tani 5620 kwa mwezi ambapo mkoa wa Kagera ulikuwa unapata tani 960 kwa mwezi (Bunazi tani 30 kwa wiki, Bukoba tani 180 kwa wiki, Ngara tani 30 kwa wiki). Mkoa wa Mwanza tani 4000 kwa mwezi kila wiki tani 1000, Kahama tani 360 kwa mwezi kila wiki tani 90, Geita tani 240 kwa mwezi kila wiki tani 60 na Kigoma tani 60 kwa mwezi.

 Aidha, Bw. Ashin Rana Alisema kutokana na viwanda vyote nchini Kilombelo, Mtibwa, na TPC pamoja na Kagera kusimamisha uzalishaji kutokana na kipindi hicho miwa shambani kuwa na maji mengi na kupelekea sukari inayozalishwa kutokana na miwa hiyo kutokidhi viwango pia muda huo unatumika kukarabati viwanda ili kujiandaa kwa msimu mpya jambo lilopelekea sukari kuwa haba nchini.
Vilevile Bw. Ashin Rana alisema kuanzia mwezi Mei 2016 uhitaji wa sukari uliongezeka na kupelekea mahitaji kuwa makubwa zaidi na mkoa wa Kagera uhitaji umepanda hadi tani 1360 kutoka tani 960 za awali kwa mwezi, kwa wiki Bukoba Tani 300, Bunazi tani 40. Uhaba huo ulipelekea uongozi wa kiwanda kupunguza kiwango cha sukari kwenda nje ya mkoa ili kukidhi mahitaji ya ndani ya mkoa.

 Baadaya ya kupunguza kiwango cha sukari inayokwenda nje ya mkoa, mkoa wa Mwanza ulianza kupatiwa tani 600 kutoka 1000 za awali kwa wiki na kwa mwezi tani 2400 kutoka 4000 za awali. Geita tani 30 kutoka 60 za awali kwa wiki na kwa mwezi tani 120 badala ya 240 za awali. Mkoa wa Kigoma zimebakia zilezile tani 60 kwa mwezi.
Bw. Ashin Rana alisema pia uongozi wa kiwanda umekuwa ukilaumiwa kuwa katika mji wa Bukoba wanaye wakala mmoja tu na kwanini wasiwe na mawakala zaidi ya mmoja. Alitoa sababu ya kuwa na wakala mmoja kuwa ni wafanyabiashara wengi wanaoomba uwakala wanaomba wakati huu sukari inapaokuawa haba ila mara baada ya viwanda vyote kuanza uzalishaji mawakala hao wanajitoa katika biashara hiyo.

 Pia aliishukuru serikali kwa ushirikiano ambao inawapatia wao kama uongozi wa kiwanda hasa katika kipindi hiki cha uhaba wa sukari. Alishukuru uongozi wa mkoa kwa kuweka mpango mzuri wa usambazaji wa sukuari ili kukidhi hasa mahitaji ya mkoa wa kagera na pia kuisambazia mikoa ya jirani kama Kigoma, Mwanza, Geita na Shinyanga.
 Mkuu wa mkoa mara baada ya kupokea taarifa hiyo alitembelea kiwanda ambacho tayari kimeanza uzalishaji aidha, alitemblea stoo ya kiwanda hicho kuijionea akiba ya sukari iliyopo na baadae alitembelea mashamba kuona jinsi kiwanda hicho kinavyoendesha kilimo cha kisasa kabisa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kuandaa na kulima mashamba ya miwa.
Akihitimisha kwa majumuisho Mhe. Kijuu aliushukuru uongozi wa kiwanda kwa kuendelea kuwasaidia wananchi hasa kwa kipindi chote ambacho sukari ilikuwa haba lakini Mkoa wa Kagera palikuwa afadhali ukilinganisha na mikoa mingine. Aidha alimulekeza Meneja Mkuu kuhakikiksha wanaendelea na uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya wananchi hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

 Naye Meneja Mkuu Bw. Ashin Rana alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2016 tatizo la sukari nchini litakuwa limeisha kwani viwanda vyote vinne tayari vitakuwa vimeanza uzalishaji wa sukari. Kwa sasa sukari yote inayozalishwa kiwandani Kagera inazalishwa na kutoka kwa kuwa bado kuna uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo ndani ya mkoa na nje ya mkoa wa Kagera.
Next Post Previous Post
Bukobawadau