Bukobawadau

SIMULIZI NDOTO ILIYOZIMWA GHAFLA

NDOTO ILIYOZIMWA GHAFLA
Na Mary Gaston:

Kulikuwa na familia moja maskini sana. Ilikuwa familia ndogo ya baba, mama na binti yao wa pekee . Baba ndiye alikuwa mtu pekee mwenye kipato, hata hivyo kipato chake kilikuwa kidogo sanaa kilichoweza kuwasaidia kujikimu mahitaji muhimu tu japo pia hakikutosha. Baba alimpenda sana binti yake na alijitahidi sana kufanya kazi za vibarua ili apate pesa za kumsomesha mwanaye aliyekuwa na ndoto za kuwa daktari. Alimpenda binti yake sana tena sana. Binti yake alikuwa na uwezo mzuri darasani, alifaulu mitihani yake kwa max za juu sana, kila mtu alimpenda kwa uwezo wake.

Ilikuwa ni siku ya matokeo yake ya shule ya sekondari kidato cha sita. Kwa mara nyingine alikuwa amefaulu vizuri kama kawaida yake, Baba yake alifurahi mno akamtaka mwanae aombe chochote kile anachokitaka kama zawadi atamnunulia. Binti akamwambia, " baba nataka gauni ambayo nilikuonyesha siku ile tulipokwenda kutembea, siku ile nilishindwa kukwambia kwakuwa gharama yake ni kubwa mno, elfu 50. Lakini kwakuwa leo umeniruhusu kuomba chochote kama zawadi nimechagua gauni." Baba yake hakujali ukubwa wa gharama, alichotaka ni kumuona binti yake wa pekee akiwa na furaha. Hivyo akaahidi kumnunulia. Kesho yake akaenda mjini akarudi na gauni la binti yake. Mke wake alijua fika mume wake hakuwa na fedha za kumudu kununua gauni hivyo akamuuliza wapi amepata kiasi hicho kikubwa cha pesa. Baba akajibu, "Nilikuwa na akiba kidogo lakini pia nikaamua kwenda hospitali kuuzwa damu yangu ili nipate fedha za kuongezea kununua gauni, sikutaka kumfedhehesha binti yangu"

Muda ukapita, binti akaanza chuo kikuu cha udaktari. Baba yake aliuza karibu kila kitu ili kulipia gharama za chuo. Aliuza vitu vyote vya ndani hadi kitanda wakabaki wanalala chini. Aliyafanya yote hayo kwakuwa alimpenda sana binti yake na alitamani kuona ndoto za mwanae za kuwa daktari zinatimia. Binti akasoma, hatimaye mwaka wake wa mwisho wa masomo ukafika. Wakati anakaribia kuanza mitihani ikaonekana kuwa hajamaliza kulipa ada, hivyo hataweza kufanya mitihani. Sasa baba hakuwa kitu cha ziada cha kuuza, hatahivyo hakutaka kumuangusha binti yake. Akaondoka akarudi kesho yake na kiasi cha fedha cha kutosha, akampa binti yake akalipe ada. Lakini tena Mke wake akagundua wazi kuwa mumewe hakuwa na fedha wala sehemu ya haraka ya kupata fedha nyingi kiasi kile, hivyo akamuuliza wapi amezipata fedha zile. Baba akajibu, "Sijafanya jambo baya, sikutaka kumuangusha mwanangu. Kuna tajiri alikuwa na matatizo ya figo hospitali, hivyo alitakiwa kupewa figo mpya maana figo yake ilikufa, nikaamua kumuuzia figo yangu moja ili nipate pesa kwaajili ya binti yangu, lakini tafadhali usimwambie, atajihisi mwenye hatia akijua nilifanya hivi kwaajili yake. " Mke wake alisikitika kwakuwa alijua figo aliyoitoa mume wake ni nzima lakini hiyo moja iliyobaki ina matatizo kwahiyo inaweza kufeli muda wowote. Kweli, muda si mrefu baba alianza kuumwa. Baba alidhoofu, alikonda sana. Alimuomba Mungu asife mpaka ashuhudie Siku ambayo mwanae anavalishwa taji na kukabidhiwa cheti chake cha heshima cha Udaktari.

Siku ikafika, ilikuwa ni siku ya Mahafali. Baba na mama walijiandaa kwa furaha kumpokea binti yao. Waliandaa kasherehe kadogo ka familia kumpongeza binti yao. Walimsubiria kwa hamu daktari mpya. Muda ukawadia, Binti akaja, ndiyo binti alikuja LAKINI alikuja kama Maiti....Ndiyo alikuwa Maiti, amebebwa kwenye jeneza!!....Usiku wa kuamkia siku ile ya mahafali alimfumania mpenzi wake, hakuwa tayari kuuvumilia usaliti ule, akaamua kunywa sumu, akaamua kuukatisha uhai wake!!. Ndoto zote zikazima ghafla. Hakuna aliyeamini tukio lile. Baba aliumia sana kumuona binti yake mpendwa akiwa maiti, akapata mshtuko wa moyo, akafariki palepale. Misiba miwili kwa siku moja.

FUNDISHO: Mara nyingi tunafanya maamuzi bila kujua ni kwa kiasi gani yatawaathiri wale wanaotupenda kwa dhati, wale wanao tumia muda wao mwingi kutupa furaha. Tunaharibu mwelekeo wetu wa maisha sababu ya kufanya maamuzi yasiyo sahihi katika maisha. Tunawafurahisha wale wasiojua thamani yetu na kuwaumiza wale wanaotuthamini kwa kila hali. Mungu akupe kufanya maamuzi sahihi, maamuzi ya kukupa wewe furaha na sio kuwapa wengine furaha wakati hawaithamini.

We only live once.
Make any decision at your own risk.

SHARE na LIKE Ukurasa wetu wa Bukobawadau Entertainment Media
Next Post Previous Post
Bukobawadau