Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AWAAGIZA VIONGOZI MKOANI HUMO KUSIMAMIA HUDUMA ZA AFYA KIKAMILIFU



MKUU WA MKOA WA KAGERA AWAAGIZA VIONGOZI MKOANI HUMO KUSIMAMIA HUDUMA ZA AFYA KIKAMILIFU
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu awaagiza viongozi katika Halmashauri za Wilaya kuchukukua jukumu la kusimamia kikamilifu shughuli mbalimbali za afya katika  Mkao wa Kagera  ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kikamilifu katika jamii.
Mhe. Kijuu alitoa agizo hilo wakati akifungua kikao cha wadau wa afya Agosti 23, 2016 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera  kilichowahusisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya na Wadau mbalimbali wa Serikali na wasiokuwa wa Serikali wanaoshirikiana katika kutoa huduma mbalimbali za afya Kagera.
Katika Agizo hilo Mkuu wa Mkoa alisistiza mambo makuu na muhimu matatu kama ifuatavyo; Kwanza aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha wanajadili kwa kina na kuweka mikakati ya kutoa huduma ya chanjo  katika Halmashauri za Wilaya ili ziweze kufikia asilimia 95% ya Kitaifa .
Pili ni kuhakikisha viongozi wanapitishwa na kuelimishwa kwa undani zaidi na wataalamu wa afya kuhusu vigezo vilivyotolewa na wafadhili wanaotoa fedha za Busket Fundi ili kushirikiana katika usimamizi kwenye Halmashauri za Wilaya kukamilisha mahitaji ya vigezo hivyo ili zikidhi vigezo hivyo na kupata fedha za wafadhili zikawahudumie wananchi kupitia sekta ya afya.
Mhe. Kijuu alisema kuwa katika majaribio ya awali yaliyofanyika katika kutathmini vigezo hivyo ilionyesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ilipata asilimia 93%, Muleba 83%, Bukoba 14% aidha Biharamulo ilipata asilimia 0% (sifuri)  na Halmashauri nyingine kutokana na wataalam wa afya kutoingiza takwimu za afya katika mfumo wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Mhe. Kijuu pia aliwakumbusha viongozi hao kuhakikisha wanasimamia na kuchukua tahadhali zote juu ya kupunguza vifo vya mama na mtoto ambapo aliagiza vituo vyote vya afya hapa Mkoani Kagera kuanza kutoa huduma za upasuaji wa dharura  kwa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijaanza kutoa huduma hiyo zianze mara moja, pia kuimarisha Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ili kupata fedha za tele kwa tele.
Naye Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Kagera Dk. Thomas Rutachunzibwa aliwashukuru wadau wote wa afya wa Mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma za afya Mkoani Kagera zinaimarika na aliwaomba kuendelea na ushirikiano wao mzuri ili kuboresha afya za wananchi wa Mkoa wa Kagera .
Next Post Previous Post
Bukobawadau