Bukobawadau

NAIBU WAZIRI STELLA MANYANYA AZINDUA RASMI MAFUNZO YA KKK KWA WALIMU 1770 MKOANI KAGERA

Mhandisi Stella Manyanya Akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius Msole Wakiwasikiliza Walimu wa KKK
 Mhandisi Stella Manyanya Mara Baada ya Kuzindua Rasmi Mafunzo ya KKK Kagera Akishuka Ngazi kuondoka.JPG
 Naibu  Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhe. Stalla Manyanya Akitoa Hotuba ya Uzinduzi
 Walimu Waliohudhuria Mafunzo ya KKK Mkoani Kagera Wakiimba Wimbo wa Mbele ya Mhe. Mhandisi Stella Manyanya
Walimu Waliohudhuria Mafunzo ya KKK Mkoani Kagera Wakiimba Wimbo wa Mbele ya Mhe. Mhandisi Stella Manyanya


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya azindua rasmi mafunzo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa walimu 1770 wa Shule za Msingi 885 za Halmashauri nane za Mkoa wa Kagera  wanaofundisha masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hisabati kwa darasa la tatu na la nne.
Akizindua mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Veta Mkoani Kagera kilichopo katika Manispaa ya Bukoba Mhandisi Manyanya aliwapongeza walimu waliohudhuria awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yaliyoanza Agosti 1, 2016 kutoka katika Halmashauri za Wilaya za Karagwe na Bukoba kwa kuitikia wito wa mafunzo hayo kwa asilimia 99%.
Pia aliwasistiza walimu hao kuzingatia mafunzo kwa umakini kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha walimu hao wanatoa elimu bora kwa wanafunzi ambapo mwanafunzi yeyote hawezi kupata elimu iliyobora kama hajui kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) masomo ambayo ndiyo msingi wa kujifunza.
Mhandisi Manyanya alisema kuwa mafunzo ya (KKK) yanaendeshwa katika mikoa 19 ya Tanzania Bara na jumla ya walimu 22995 watapatiwa mafunzo hayo ukiwemo Mkoa wa Kagera utakaonufaika kwa mafunzo hayo kwa walimu 1770 ambao wanatarajiwa kuwanufaisha pia walimu wenzao kwa mafunzo hayo ya (KKK) pindi warejeapo shuleni kwao.
Ombi, Mhandisi Manyanya aliwaomba walimu hao pia kuanzisha madarasa ya watu wazima ili kutoa fursa kwa wananchi ambao hawakuweza kupata elimu ya msingi ili na wao wafundishe kusoma, kuandika na kuhesabu. “Kwa takwimu za Sensa ya mwaka 2012 ilionekana kuwa bado asilimia 29% ya wananchi kuanzia umri wa miaka 8 hadi 50 hawajui kusoma na kuandika kwahiyo nawaombeni sana tusaidiane kuondoa tatizo hili nchini kwetu.” Aliwaomba walimu hao Mhandisi Manyanya.
Aidha, Mhandisi Manyanya alibainisha kuwa nia ya Serikali ya kujenga Chuo cha VETA cha kisasa Mkoani Kagera katika eneo la Burugo bado ipo palepale kwani imetengwa fedha katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 ili watoto watakaokuwa wanamaliza elimu ya Msingi na Sekondari wakapate ujuzi wa ufundi chuoni hapo.
Katika Hatua Nyingine Bw. Benard Merumba Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Bagamoyo (ADEM) alisema  mafunzo ya (KKK) yanalenga kuwafundisha walimu kutambua na kuelewa Sera mpya ya Elimu ya Mwaka 2016, Kuitambua na kuielewa miongozo ya kufundishia masomo husika.
Vilevile walimu kukutambua mbinu sahihi za kujifunza na kufundisha pamoja na upimaji wa ufanisi wa mada zinazotolewa kwakutumia mbinu shirikishi. Bw.Merumba alisema pia kuwa mafunzo hayo yanaendeshwa na wakufunzi 32 kutoka katika vyuo mbalimbali nchini.
Naye Mwalimu Fides Mnyogwa alisema kuwa anaishukuru Serikali kwa kuliona hilo na kutoa mafunzo hayo hasa kuhusu mitaala kwa walimu wanaofundisha masomo ya Kiswahili, kiingereza na Hisabati kwani hapo awali walimu walikuwa wanafundisha wanavyojua kila mmoja, lakini mara baada ya kupata mafuzo hayo sasa watapata uelewa wa pamoja na kufundisha kwa mbinu sahihi za aina moja.
Mafunzo yanatarajia kukamilika Septemba 15, 2016 mara baada ya Walimu kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Kagera kupata mafunzo hayo ya (KKK).
Next Post Previous Post
Bukobawadau