Bukobawadau

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 04 AGOSTI, 2O16

Ndugu Waandishi wa Habari, Katika Mkoa wetu wa Kagera vimeibuka vitendo vya hujuma hasa wakati huu wa majira ya kiangazi (hususani mwezi Juni na Julai 2016) ambapo wananchi wenye nia mbaya na Taifa na Mkoa wetu wamekuwa wakichoma moto ovyo na kuteketeza misitu ya hifadhi ya Serikali, mashamba ya miti ya watu binafsi na mashamba ya mazao ya chakula suala ambalo halikubaliki na ni kinyume na sheria zilizowekwa na nchi yetu.
Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa taarifa nilizonazo za uchomaji moto katika Halmashauri za Wilaya tatu mkoani kwetu ni kama ifuatavyo; Kufikia Agosti 3, 2016 katika Manispaa ya Bukoba maeneo yaliyoripotiwa kuchomwa moto ni ekari tisa na nusu (9.5) zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni ishirini (20,000,000)
 Katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba zaidi ya ekari 473 za misitu ya hifadhi ya kupandwa na mazao ya chakula imechomwa na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo taarifa zilizonifikia ni kwamba tayari ekari 53 za misitu na mazao ya chakula zimechomwa na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha pia kwa wananchi. Kwa hizo Halmashauri chache za Mkoa wa Kagera unaweza kuona uharibifu mkubwa wa uchomaji moto ulivyosababisha hasara kubwa.

Ndugu Waandishi wa Habari, Kutokana na uharibifu huo wa uchomaji moto katika Mkoa wetu wa Kagera na kwa Mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha sheria ya Tawala za Mikoa, sheria Na. 19 ya mwaka 1997 Kifungu cha 5 kifungu kidogo cha (1) na (2), Sheria hii inanipa Mamlaka na majukumu ya kulinda Amani na Usalama na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria katika Mkoa wa Kagera unatimizwa. 
 Aidha, kwa kuzingatia sheria ya misitu Na. 14 ya mwaka 2002 vifungu vya 70 hadi 73 na Kifungu cha 91 vifungu kidogo (1) na (2) vinavyozuia mtu yeyote kuchoma mashamba binafsi na misitu ya hifadhi. Hivyo, ninawaagiza Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wote Mkoani Kagera kuhakikisha wanadhibiti uchomaji moto ovyo kwenye Wilaya zao kwa kutumia sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na sheria ndogo za Halmashauri za Wilaya za utunzaji wa mazingira.
Ndugu Waandishi wa Habari, Aidha, naagiza kwa maeneo ambayo yatabainika kuchomwa moto, moto huo uzimwe mara moja kwa ushirikiano wa wananchi na kumbaini mara moja mwananchi aliyehusika kuchoma moto huo katika eneo husika.
 Pia naagiza Viongozi wote kuanzia ngazi ya Kitongoji,Kijiji,Kata,Tarafa na Wilaya wenye jukumu la kisheria kusimamia misitu na mazingira wahakikishe waharifu wa uchomaji moto wanabainika na kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, Viongozi watakaoshindwa kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Ndugu Waandishi wa Habari, Vile vile naagiza Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha taarifa za kudhibiti uchomaji moto na kubaini waharifu wa uchomaji moto ovyo zitumwe Ofisini kwangu kila siku. Pia Kamati za Mazingira zilizoundwa kupitia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kwa ngazi zote zihakikishe zinatekeleza kazi zake kisheria na kuwasilisha taarifa Mkoani kila Wiki.
Ndugu Waandishi wa Habari, Nawakumbusheni kuwa Misitu ni rasilimali muhimu kwa Taifa na kwa Mkoa wetu wa Kagera kwani misitu ni uhai. Misitu huchangia kuwepo kwa hali nzuri ya hewa, uwepo wa mvua za uhakika na uwepo wa vyanzo vya maji vya kutosha Mkoani kwetu na Taifa kwa ujumla.
 Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 inaitambua misitu ya hifadhi ya asili na ile ya kupandwa na inaeleza wazi ni jukumu la kila Mwananchi kuhakikisha misitu hii inalindwa na kutunzwa. Nawakumbusheni wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na kuacha vitendo vya uchomaji moto ovyo katika mkoa wetu wa Kagera badala yake wanatakiwa kuwa walinzi mazingira katika maeneo yao.
Imetolewa na; Mhe. Meja Jenerali (Mst) Salum M. Kijuu
Mkuu wa Mkoa
KAGERA
Next Post Previous Post
Bukobawadau