23 May 2013
RAIS KIKWETE ATOA MSIMAMO MKALI KUHUSU VURUGU MTWARA
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amekemea vikali vurugu zilizotokea jana mkoani Mtwara baada ya kusomwa bungeni kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Akizungumza katika eneo la Kizota, Dodoma wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Dodoma kwenda Iringa, Rais Kikwete alisema wote waliohusika na vurugu hizo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali.
Rais Kikwete alisema rasilimali inayopatikana mahali popote pale nchini inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote... “Hivi watu wa Nyarugusu wadai dhahabu ya pale au kinachopatikana Chalinze basi kisitumiwe na watu wa Morogoro! Hivi tutakuwa na taifa kweli?,” alihoji kwa ukali Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa Serikali itawasaka wale wote wanaoongoza vurugu hizo na watawajibishwa kwa makosa hayo... “Tutawasaka hawa watu na viongozi wao hata kama wana mapembe kiasi gani, tutayakata.”
Alichosema Waziri Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mradi wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, umeanza kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakwenda huko wiki ijayo kuweka jiwe la msingi.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini jana, Waziri Muhongo alisema:
“Mradi wa kujenga bomba la gesi uko palepale na unaendelea kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ataenda kuweka jiwe la msingi wiki lijalo.”
“Tumezungumza mengi kuhusu suala hilo na hata viongozi wa watu wa Mtwara walipelekwa nje kujifunza faida zake, lakini hata kama hawajaelewa, nimetoa kijitabu kinachozungumzia faida mbalimbali watakazopata wana Mtwara katika mradi huo.”
Profesa aliyeanza hotuba yake kwa kueleza machapisho mbalimbali yaliyotolewa na wizara yake kufafanua faida za gesi ya Mtwara kwa taifa, alisema mradi huo uliozinduliwa Novemba mwaka jana na Rais Kikwete, unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 532 na kipenyo cha nchi 36.
“Bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha futi za ujazo za gesi milioni 784 kwa siku. Mradi utahusisha mitambo miwili ya kusafirisha gesi asilia katika maeneo ya Mnazi Bay- Madimba (Mtwara) na Kisiwa cha Songosongo (Lindi). Utagharimu Dola za Marekani 1,225.3 milioni,” alisema.
Alisema kazi za usanifu wa mradi na ulipaji fidia kwa wananchi wapatao 3,092 waliopisha maeneo ya mradi, zimekamilika na hatua za awali za ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi asilia zimeanza.
| Reactions: |
Waziri akiri kuhusu mbolea feki nchini
| Reactions: |
HAYAWIHAYAWI, SASA YAMEKUWA! USIKU WA HIP HOP, THE VODACOM MIC KING KURINDIMA J’MOSI HII DAR LIVE
Wakali tisa wa Hip Hop wanaowania gari aina ya Toyota FunCargo (new model), katika pozi mbele ya gari lao.
Na Mwandishi Wetu
ILIPANGWA, ikapangika. Baada ya kusubiririwa kwa muda mrefu, hatimaye msimu mpya wa shoo ya Usiku wa Hip Hop (2013) unachukuwa nafasi Jumamosi hii ndani ya Ukumbi wa Dar live, Mbagala-Zakhem, jijini Dar.
Wasanii wanaotamba kwenye gemu la Hip Hop, Kala Jeremiah, Fid Q, Nay wa Mitego, Joh Makini, Stamina na wengine kibao pamoja na washiriki wa Shindano la The Vodacom Mic King watakamua shoo baab’kubwa kuweka historia mpya ya burudani.
Meneja Matukio wa Ukumbi wa Dar Live, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ amewahakikishia mashabiki wote wa muziki wa Hip Hop kuwa Jumamosi kutasheheni matukio kibao, ulinzi mzito utakuwepo pamoja na parking kubwa ya magari hivyo watu wafike kwa wingi watainjoi kwa nafasi na kuondoka salama ukumbini.
“Vijana tisa waliosalia katika Shindano la The Vodacom Mic King watapanda jukwaani na kushusha mistari ambapo mshiriki mmoja anatarajiwa kuondoka na gari jipya aina ya Toyota FunCargo (new model),” alisema Abby Cool na kuongeza:
“Mashabiki wanaweza kulifuatilia shindano hilo kupitia Runinga ya DTV kuweza kujua jinsi ya kuwapigia kura.”
Washiriki hao na namba zao za ushiriki kwenye mabano ni Ally (MK 02), Anold (MK 03), Bahati (MK 05), Boniface (MK 07), Emmanuel (MK 10), Ibrahim (MK 12), Karrys (MK 13), Lusajo (MK 14) na Martin (MK15). Jinsi ya kuwapigia kura, wasomaji wanatakiwa kuandika neno MK wakiambatanisha na namba ya mshiriki kisha kutuma ujumbe huo kwenda namba 15564.
OFA ZAIDI KWA MSHINDI
Mbali na mshindi kuondoka na gari, Mrisho aliongeza kuwa washindi watatu wa nafasi za juu watajipatia dili la kurekodi singo mojamoja kutoka kwa prodyuza kiwango aliyezalisha ngoma kali Bongo ikiwemo ya Kundi la Kigoma All Stars iitwayo Leka Dutigite, Tudd Thomas.
TUZO KUTOLEWA
Mrisho alitiririka na mistari kuwa, mbali na shoo kali kutoka kwa wakali hao wa Hip Hop, kutakuwa na kipengele cha kutoa tuzo za muziki wa Hip Hop katika vipengele tofauti hivyo mashabiki pia waendelee kuwapigia kura wasanii wanaowapenda.
Vipengele vitakavyotolewa tuzo ni Mwanamuziki Bora wa Hip Hop (Legendary) ambapo yamepita majina matatu; Fid Q, Joh Makini na Profesa Jay. Pia kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Hip Hop (Chipukizi) ambacho kina majina kama Young Killer, P The Mc na Tabla huku akianisha kipengele cha mwisho ambacho ni Wimbo Bora wa Hip Hop (2012/13) chenye nyimbo kali za Dear God (Kala Jeremiah), Sihitaji Marafiki (Fid Q) na Najuta Kubalehe (Stamina).
“Ili kuwapigia kura, mashabiki wanatakiwa kuandika neno BHL wakiambatanisha na jina la msanii husika kwenda namba 15564 katika kipengele cha Msanii Bora wa Hip Hop (Legendary).
“Kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Hip Hop (Chipukizi), mashabiki waandike neno BUA na kufuatiwa na jina la msanii wanayempenda kwenda namba 15564,” alisema Abby Cool na kuongeza:
“Kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka, mashabiki waandike neno BHS likifuatiwa na jina la msanii wanayempenda kisha watume ujumbe huo kwenda namba 15564.”
KUWAENZI WASANII/SOKA KWENYE SKRINI KUBWA
Abby Cool aliweka bayana kuwa katika shoo hiyo kutakuwepo na documentary maalumu ya kuwakumbuka wasanii wa Hip Hop waliotangulia mbele za haki kupitia skrini kubwa bila kusahau mashabiki wa soka watapata fursa ya kushuhudia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa) kati ya Bayern Munich na Borrusia Dortmund. Twendeni Dar Live J’mosi!
| Reactions: |
22 May 2013
HALI SI HALI UKO MTWARA. Katika tukio lingine askari wanne wa jeshi la wananchi kikosi cha 41 KJ wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa baada ya gari lao kupinduka eneo la Kilimani hewa Nachingwea njiani kuelekea Mtwara kuongezea nguvu jeshi la polisi kufuatia vurugu zilizotokea mkoani humo
Ambulance ya Manispaa ndiyo hivyo tena.
Yanaonekana Magari ya Watumishi yakiteketea kwa moto.
Hali
Mtwara bado ni tete: ITV wameripoti muda si mrefu kuwa jengo la CCM
Wilaya ya Mtwara limeteketezwa kwa moto, baada ya kupigwa kiberiti na
watu wasiojulikana.Spika kasema amepokea hali ya vurugu Mtwara, hivyo bunge limeahirishwa ili kutoa fursa kwa kamati ya bunge kujadili suala hilo na serikali imetakiwa kutoa majibu katika kikao cha kesho.
Spika kasema kuwa wabunge wangependa kujadili hali ya Mtwara leo lakini watajadili nini wakati hata wao wabunge wamepata taarifa hizo kwenye vyombo vya habari? Hivyo, akaiagiza serikali kuleta majibu sahihi kesho bungeni na kuwaomba wabunge kuwa na subira hadi kesho na kisha akaahirisha bunge. Akahitimisha kwa kusema kamati ya bunge inakwenda kujadili suala hilo sasa hivi.
Katika vurugu hizo tairi zimechomwa barabarani kuzuia njia kupitika
| Reactions: |
KUTOKA JF HIZI NI Fikra Mbadala: # Lowassa kama Rais itakuwa ni Kikwete 2.0 (Marudio ya 2005)
Kashfa ya Richmond kama alivyosema Kikwete mbele ya wazee wa Dar ilikuwa ni "ajali ya kisiasa" tu kwa Lowassa. Ilikuwa ni ajali mbaya hata hivyo kwa sababu ilivuruga kwa kiasi kikubwa na imeacha ombwe kubwa sana la kujijenga tena Lowassa. Lakini halikufuta ndoto ya yeye kuutaka Urais; wengine wanaweza kusema ni "haki" yake; aliahidiwa kupokezana; anatoka Kikwete anaingia Lowassa.
Je, utawala wa Lowassa unaweza kuwa tofauti? Well, je nyani akiamua kuondoka shambani na kuwaachia ngedele mahindi yatakuwa salama? Kufikiria kuwa CCM chini ya Lowassa na Tanzania chini ya Lowassa itakuwa tofauti ni kujaribu kukinga mikono jangwani kungojea mvua.
Kwa ufupi, yeyote anayetaka mwendelezo wa utawala wa Kikwete kwa miaka kumi ijayo - ndani ya CCM na kwa taifa - uchaguzi uko wazi - kuhakikisha kuwa Lowassa anachaguliwa kuwa Rais. AU watu watuambie utawala wa Lowassa utakuwa na tofauti gani na utawala wa Kikwete na kwanini?
| Reactions: |
FANI YA UANDISHI WA HABARI IMEVAMIWA, TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA.
Watu wengi kwa sasa wameibuka na kutokea kuipenda fani ya uandishi wa habari bila kujua misingi na miiko ya uandishi wa habari. Tatizo moja ambalo limeonekana ni kubwa sana ni utandawazi ambao umekuwepo na kutokea ibuko la kila kijana kufungua gazeti tando (blog).

| Reactions: |
SHANGWE ZA UZINDUZI WA VISION MUSIC AMBASSADOR NDANI YA BUKOBA CLUB
Wanasema msanii ni kioo cha jamii na anaweza kuelimisha jamii kwa kupitia nyimbo zake ,ndivyo alivyofanya RISING STAR wa KAGERA mzaliwa NKAKA KIJUNJA KASHASHA katika familia ya Ngemela chimbuko la Itembwe's ni OMG SHEMELA akiimba nyimbo yake inayofanya vyema katika radio stadion mbalimbali nchini iitwayo AFRIKA!!!
Anaitwa Bk Sunday, ni msanii kutoka Wilayani Muleba aliye jipatia umaarufu mkubwa kanda ya ziwa kwa kibao chake maarufu kama ASSECDO.
Picha kwa hisani ya Vision Fm Radio
| Reactions: |
21 May 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:CCM yakanusha uvumi wa Kikwete kuruhusu wagombea kuanza kampeni!
Kikao hicho kilikuwa na lengo la wabunge wa CCM na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia ni Rais na mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kubadilishana uzoefu wa namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa kipindi cha nusu ya muhula wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo uliwekwa mwelekeo wa namna bora ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa kipindi kilichobaki.
Kwahiyo kwa kifupi lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa ilani majimboni na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha ilani na ahadi za CCM na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo baada ya semina hiyo baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Kikwete kuwa ameruhusu wanaokusudia kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015 kufanya kampeni.
CCM imesikitishwa na nukuu hiyo ya kupotosha ukweli wa kilichojadiliwa na hivyo tumelazimika kutoa ukweli wa kilichojiri na kujadiliwa. Ni kweli kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali wanaotajwa au wanaojitaja kuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani, ubunge na Urais ulikuwepo na ulikuwa mkali.
Hata hivyo hitimisho la kikao na majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM Taifa lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika hizo na uvunjifu huu wa makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi pirika hizi zinakigawa Chama na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha watu wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya waandishi, uhuni huo haukubaliki.
CCM ina kanuni na taratibu zake zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi taifa.
Kanuni hizo ni pamoja na kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012.
Katika Kanuni za Uchaguzi wa CCM Toleo la 2012 kanuni za jumla Ibara ya 33 inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa wakati wa shughuli za uteuzi na uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na wale wote wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-
(1). “….wanachama wenye nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa na kikao kinachohusika”.
(4). “Ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”.
Ibara hiyo ya 33 kifungu kidogo cha 1 na 4 vinaweka wazi msimamo wa kikanuni wa Chama. Hivyo basi kwa mujibu wa kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na wabunge wa CCM mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;
Ni marufuku kwa mwanachama yeyote wa CCM anayetaka kuomba CCM impe nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha na kuita wapiga kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali zitachukuliwa kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.
Lakini pia ni marufuku kwa viongozi na watendaji wa Chama kujihusisha na kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye nia ya kugombea kupitia CCM kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi na watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.
Tunawataka wote wenye nia, viongozi na watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele ya safari.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
| Reactions: |
PICHA NA MATUKIO MBALIMBALI
Hivi ndivyo Msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, Joseph Haule, (Prof. Jay) alivyo jiunga rasmi leo na chama cha CHADEMA.
NYEPESI NYEPESI TULIZONAZO JUU YA UJIO WA JIGGAR
Bado wataalam wa mambo wanaendelea kutofautiana kuhusu ratiba ya Tour ya Jay – z iliyotolewa na Billboard hivi karibuni katika ratiba hiyo imeandikwa Jay z atatua katika miji 7 ya Africa ikiwemo jiji la Dar es salaam Oktoba 4 mwaka huu pale Diamond Jubilee. Ratiba hiyo inatia shaka kwa sababu Jay z aliperform tarehe na mwezi kama huo Dar es salaam mwaka 2006 na katika website ya Jay za ametoa ratiba ya Tour zake lakini ameishia kuandika mwezi Septemba, hajaandika mpaka Oktoba kama walivyoandika Billboard
Tanzania imepata hasara ya dola bilioni 1.8 za kimarekani kwa mwaka jana kutokana na ukosefu wa ufanisi bora katika bandari ya Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya benki ya dunia kama hatua za kuboresha ufanisi katika bandari hiyo zitachukuliwa na rushwa ikapungua ,uchumi wa tanzania utainuka kwa kiasi kikubwa.
MJINI BUKOBA Wajanja wote wanasikiliza Vision fm radio 100.OMHz kutoka KIBETA, BUKOBA-TANZANIA karibu utusikilize katika msimu huu mpya wa mapinduzi ya utangazaji na masuala mazima yanayohusu burudani hapa Kagera na tuunge mkono kwenye kampeni ya kuinua uchumi na maendeleo ya wana Kagera na hasa Vijana ambao ndio taifa la leo ambalo mara zote wamekuwa na changamoto nyingi za kuanza maisha na kuyafanya kuwa "BORA"
VISION FM RADIO 100.0MHz "ONGEZA MTAZAMO"
Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anna Kilango akizozana na mnadhumu wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu nje ya ukumbi wa Bunge baada ya Spika kuahirisha Bunge akiagiza hotuba ya kambi ya upinzani kuhusu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kufanyiwa marekebisho.Picha na Emmanuel Herman
| Reactions: |
SIRI YAFICHUKA KIFO CHA KAMANDA BARLOW;Polisi Muna atajwa, Mh. Pinda atoa maelekezo baada ya kupewa taarifa.
Kuvuja kwa siri hiyo kumetokana na mmoja wa jambazi sugu ajulikanaye kwa jina la Edward Malele kujisalimisha ktk vyombo vya ulinzi na kutoa siri zote.
Jambazi huyu aliombwa wa genge ndani ya polisi kushiriki katika mpango wa kumwua kamanda Barlow. Akakataa kwa kuwa aliwahi kumfahamu kwa karibu kamanda Barlow.
Baada ya kukataa kutekeleza agizo hilo baada ya siku chache alishtakiwa kwa kosa la ujambazi na kuswekwa Rumande.
Akiwa huko ndani ya wiki moja alisikia habari za kifo cha kamanda Barlow. Akajua akina Muna aliowakatalia wamefanya kazi aliyoikataa yeye. Na alijua yuko mahabusu kwa sababu ya kukataa mradi huo.
Baada ya kukaa huko muda mrefu bila shitaka kueleweka wala mshataki wake, huko Lupango walimua kumwaichia, Akagoma kutoka kwa sababu anajua kuwa, kwa kuwa amepelekwa huko ili kuficha siri hivyo, akitoka lazima atauawa. Baada ya muda akaamua kukubali kutoka lupango na kukimbilia kituo cha JWTZ huko Mwanza.
Huko JWTZ Alijieleza vya kutosha na wanajeshi walimwonea huruma wakampa Nauli na Tsh 10,000/= ya kula njiani ilie aende Bungeni huku wakiwa wamemkabidhi namba za simu za wabunge 2 wa upinzani ili wamsaidie.
Kutokana na kutokuelewa kwake alipokuwa anashangaa shangaa katika eneo la Bunge, alikamatwa na polisi wanaolinda eneo hilo. Polisi hao wakapiga simu Dodoma central na Mwanza. Haraka haraka mwanza wakataka arudishwe mwanza kwa kuwa ni jambazi sugu.
Hata hivyo katika kurupushani hiyo taarifa zimesha mfikia Waziri Mkuu Mh.Pinda na Nchimbi ambapo gazeti linaripoti kuwa Pinda ameagiza kijana huyo apewe ulinzi na asirudishwe Mwanza.
Hata hivyo amepelekwa kusiko julikana.
Kwa mapana zaidi soma gazeti la Jamhuri na zinanunuliwa kwa kasi na watu wasiofahamika
Source JF.
| Reactions: |
HALI SI HALI MATOKEO KIDATO CHA SITA: Sifuri kibao zafutwa kimya kimya!
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ambalo linaendelea kupanga matokeo hayo ya kidato cha sita kwa kuzingatia alama za zamani kama ambavyo taarifa ya awali ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilivyosomwa bungeni hivi karibuni, hali ingekuwa mbaya zaidi katika ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kiasi cha kuweza kutishia uhai wa vyuo vikuu nchini kukosa wanafunzi wa kutosha.
“Hali ilikuwa mbaya sana kama alama za kufaulu zingeachwa zitumike zile mpya na si za zamani. Vyuo vikuu nchini visingeweza kupata wanafunzi wa kutosha. Tatizo hapa si uwezo wa wanafunzi moja kwa moja katika kumudu mitihani bali ni kufanywa kwa mabadiliko ya alama bila kuwaandaa. Alama hizi zilipaswa kuanza kutumika na wanafunzi wapya, yaani kama wanaanza kidato cha kwanza wawe wanapewa mitihani ya kupimwa kwa kuzingatia alama mpya na waendelee nazo hadi mitihano yao ya mwisho.
“Na hivyo hivyo kwa wanafunzi wa kidato cha sita. Alama hizi mpya zinapaswa kutumika kwako kuanzia wakiwa kidato cha tano mara wanapoanza shule, kila mitihani wanayopewa isahihishwe na kupangiwa alama kwa kutumia hizi alama mpya,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka NECTA.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya alama, alama mpya zilizokuwa zimetumika awali ni daraja F kuanzia 34 hadi sifuri; badala ya alama hiyo F kuanzia 20 hadi 0; daraja D kwa kuzingatia alama mpya linapaswa kuanzia 35 tofauti na awali, yaani alama 21.
Taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, kati ya sababu za kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita tofauti na muda uliotarajiwa yaani mwanzoni mwa Mei, ni pamoja na upangaji upya matokeo hayo, ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa kwa kidato cha nne ambapo matokeo yalitangazwa na kisha kufutwa ili kuyapanga upya kwa kutumia alama za zamani.
Lakini alipoulizwa kuhusu masuala hayo ndani ya NECTA, Ofisa Habari wa Taasisi hiyo nyeti nchini, John Nchimbi alisema; “Kwa sasa niseme tu kwamba mchakato wa kuandaa matokeo ya kidato cha sita unaendelea, siwezi kusema lini hasa utakamilika lakini nina uhakika ni katika muda muafaka.”
Kuhusu matokeo ya kidato cha sita kucheleweshwa kutokana kupangwa upya ili kupunguza idadi ya waliofeli kutokana na matumizi ya alama mpya za kufaulu, Nchimbi anasema; “Unajua haya maagizo haya ya bungeni (kupanga matokeo kwa kuzingatia alama za zamani) yamekuja wakati mchakato wa kuandaa matokeo ulikwishaanza. Kwa hiyo baada ya maagizo ilibidi kufanya kazi hiyo tena kwa kufuata maagizo hayo.”
Hata hivyo, hakuweka bayana kama matokeo ya awali kabla ya maagizo ya Serikali yaliyotolewa bungeni kutumia alama za zamani yamewafanya wanafunzi wengi kufeli na badala yake akasema; “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mchakato wa matokeo hayo haukuwa umefika mwisho. Takwimu rasmi hazikuwa zimekamilishwa. Kwa hiyo si sahihi kusema rasmi walifeli.”
Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa matokeo yanayotarajiwa ya kidato cha sita, taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, baada agizo la serikali la kufuta na kurejewa upya kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012, takriban wanafunzi 50,000 wamepata unafuu katika matokeo yao tofauti na awali.
Awali, kwa kuzingatia matokeo ya kidato cha nne mwaka jana yaliyotangazwa Februari, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa, jumla ya watahiniwa 126,847 tu kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Katika matokeo hayo idadi ya wasichana waliofaulu ilitajwa kuwa ni 46,181 wakati wavulana waliofaulu ikiwa wanafunzi 80,686 na idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 16,112 kati yao watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani wasichana ni 6,7751 na wavulana 9,361.
Katika matokeo hayo watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, daraja la pili 6,453 na daraja la tatu ni 15,426, wakati waliopata sifuri ni 240,903 lakini kwa kuzingatia taarifa za vyanzo vyetu ndani ya Baraza, idadi hiyo itabadilika kwa sababu ya alama kuongezwa kwa watahiniwa hao wa mwaka 2012.
Lakini matokeo hayo yalitangazwa pamoja na vituko walivyofanya baadhi ya wanafunzi, vikiwamo vituko vya kuandika matusi kwenye karatasi za majibu ya mitihani na kutokana na makosa hayo, watahiniwa 789 walifutiwa mitihiani yao.
Source Gazeti la Raia Mwema.
| Reactions: |
KINACHOMPONZA PRODYUZA TUDD THOMAS NI UCHAWI AU KUSAHAU?
MASHABIKI wa mtayarishaji wa muziki (Producer), mwenye uwezo wa kipekee, aliyetayarisha wimbo wa Leka dutigite wa Kigoma All Stars na zingine nyingi, Tudd Thomas, wamekuwa wakiulizana maswali mengi wao kwa wao pasipo kupata majibu.
Safari ya Tudd Thomas katika muziki, ilianzia mkoani Iringa akiwa Iringa Records aliporekodi wimbo wa mwanamuziki Marlaw unaoitwa Bembeleza. Wimbo huo ulipata tuzo ya wimbo bora wa mwaka kutoka Kilimanjaro Tanzania Music Awards mwaka 2008 na pia kumfanya Marlaw apate tuzo ya msanii bora wa kiume kupitia tuzo hizo. Baadae alihamia jijini Dar es Salaam na ndipo alipoonesha uwezo wake zaidi kwa kusuka nyimbo zilizotikisa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Hakuna asiyeufahamu wimbo wa Pii Pii (Missing my baby) wa Marlaw ambao aliutengeneza yeye kupitia Studio ya JML. Wimbo huo ulipata tuzo nyingi ikiwa ni pamoja na tuzo ya Nzumari nchini Kenya mwaka 2009 mbapo uliingia kwenye kipengere cha wimbo bora wa Afrika Mashariki, kumfanya Marlaw aingie kwenye kipengele cha msanii bora wa Afrika Mashariki na kunyakua tuzo hiyo. Baada ya hapo wimbo huo ulipata tuzo ya Kilimanjaro nchini Tanzania kama wimbo bora wa mwaka wa Afro pop mwaka 2010, tuzo ya Chaguo la Teneez Music nchini Kenya kama wimbo ulioongoza kwa kuchukuliwa kwa njia ya mtandao Afrika Mashariki “The most downloaded East African song” mwaka 2010, pamoja na tuzo ya Nigeria Sound City Video Music kama wimbo bora wa Afrika Mashariki mwaka 2010.
Aliendelea kutayarisha nyimbo ambazo zilipata umaarufu mkubwa na kuingia kwenye vipengele mbalimbali vya tuzo za muziki za Kilimanjaro. Mwaka 2012, nyimbo tatu zilizotokana na mikono yake zilipata nafasi ya kushiriki tuzo hizo. Nyimbo hizo ni Liz One wa Izzo Business ambao uliingia kwenye vipengele viwili ambavyo ni wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa Hip hop na pia kusababisha msanii huyo aingie kwenye kipengele cha msanii bora wa Hip hop. Milele daima wa Barnaba na Kizunguzungu wa Rachel, ambapo zote ziliingia kipengele cha wimbo bora wa Zouk/Rhumba pia ni nyimbo alizotengeneza mtayarishaji huyo.
Nyimbo zingine alizotayarisha ambazo zilifanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya redio na TV ni Kisa pombe na Soldier za Mwasiti, Sorry sana, Mbayuwayu na Mtoto wa Afrika za Marlaw pamoja na Natumaini ya Becka aliyowashirikisha Barnaba na Amin. Pia zipo nyingine kama Unikimbie ya Amin, Tushukuru kwa yote ya Ditto, Lonely ya Linah na Magubegube ya Barnaba.
Mtayarishaji huyo ambaye hajawai kuingia kwenye tuzo za Kilimanjaro za muziki wa hapa nchini Tanzania ambazo mwaka huu zimeongezewa kipengele cha Mtayarishaji bora chipukizi ndiye aliyetayarisha wimbo wa Leka dutigite wa Kigoma All Stars kupitia Studio yake ya Ngoma Records. Wimbo huu umeingia kwenye kipengele cha wimbo bora wa mwaka 2013. Pia alishirikiana na mtayarishaji Imma the boy kutengeneza wimbo wa Me ‘n’ U wa Ommy Dimpoz ambao umeingia kwenye kipengele hicho na vipengele vingine ambavyo ni wimbo bora wa Bongo Pop na wimbo bora wa kushirikiana.
Alipoulizwa alisema hapendi kuzungumzia juu ya kutotajwa kama miongoni mwa wanaowania tuzo. Aliendelea kusema kwamba, hata kama baadae ikitokea, kwake ni motisha tu, lakini kikubwa zaidi ni kwamba anahisi analo deni kubwa la kutumia uwezo wake ipasavyo kufanya kazi nzuri zaidi ya hapo ili kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa. Pia alisema ana malengo makubwa aliyojiwekea na ndiyo maana kila kukicha anawaza kutayarisha nyimbo zenye tofauti na zenye radha ya kipekee.
Tudd Thomas anaendelea kukitumia kipaji chake na ujuzi wake ipasavyo na siku chache zilizopita kuna nyimbo zisizopungua tatu zilizoingia sokoni na zinafanya vizuri, ambazo ni kazi za mikono yake. Nyimbo hizo ni Uswazi take away ya Chegge, Nyumbani ya Kigoma All Stars na pia ameshirikiana kwa kiasi kikubwa na mtayarishaji Fundi Samwel kutengeneza wimbo wa Mahakama ya mapenzi wa Linex.
| Reactions: |




















