Bukobawadau

SHEHENA YA HEROIN YAKAMATWA IKIINGIZWA NCHINI

Kikosi kazi cha Jeshi la Polisi cha Kudhibiti Uharamia Baharini kimekamata kilo 201 za dawa za kulevya aina heroini zilizokuwa zikiingizwa nchini kutoka Iran.

Kamishna wa Polisi, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema jana kikosi hicho kikiwa kwenye doria ya kawaida kiliona boti ambayo haikuwa na bendera wala kiashiria chochote ndipo walipoitilia shaka na kuamua kuifuatilia.

Nzowa alisema “mzigo huo ni mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa na vikosi vya doria vya Tanzania. Mara ya mwisho kwa mzigo mkubwa zaidi wa heroin kuwahi kukamatwa ilikuwa mwaka 2012 wakati zilipokamatwa kilo 70 za dawa hizo jijini Dar es Salaam.”

“Kikosi cha Wanamaji kiliposhuku boti hiyo, kiliisimamisha na na kuivuta hadi ufukweni. Ndani ya meli kulikuwa na watu 12; ambapo wanane ni raia wa Iran na wanne wa Pakistan. Aidha, baada ya upeuzi mkali ndani ya meli ndipo zikakutwa kilo 201 za heroin,” alisema Nzowa.

Nzowa alisema “kitakachofuata sasa ni kufanya upelelezi na kujua walikuwa wanataka kupeleka wapi mzigo huo, kufahamu mtandao wao na walipanga kufanya nini katika ufukwe wa Dar es Salaam. Baada ya upelelezi kukamilika watu hao watafikishwa mahakamani.”

Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Polisi, ACP Mboje Kanga alisema watu hao 12 hivi sasa wamewekwa mahabusu ya wanamaji na kikosi hicho kwa kushirikiana na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wataendelea na upelelezi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau