Bukobawadau

RIDHIWANI KUWA MTOTO WA RAIS HAVUI HAKI YAKE YA URAIA

Na Robert Mdoe
WANA CCM wa jimbo la Chalinze wamempendekeza Ridhiwani Kikwete kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya  chama chao. Ni katika uchaguzi mdogo utakaofanyika jimboni humo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo.
Baada ya jina la Ridhiwani kutangazwa kuwa kashinda kura za maoni, tena kwa kishindo, ili kupeperusha  bendera ya chama chake katika uchaguzi huo mdogo, maneno yameanza kutoka kona mbalimbali kuwa huyo kapata nafasi hiyo kwa vile  ni mtoto wa kigogo, mtoto wa rais aliye pia mwenyekiti wa CCM! Wengine wakisema kwamba  kwa vile Kikwete  amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo hivyo haikufaa mwanae naye awe mbunge wa jimbo hilohilo eti katika kuliepusha lisionekane linaongozwa katika mfumo wa kiukoo!
Makala nyingi zimeandikwa katika magazeti mbalimbali zikikishangaa na nyingine zikikilaani kitu hicho cha Ridhiwani kupendekezwa na wanachama wa chama chake kuwa mgombea wao katika jimbo hilo.
Kuna makala niliyoisoma katika gazeti la kila wiki ikisema “Ridhiwani, Mgimwa na ujio wa nepotism Tanzania”. Makala hiyo inausakama ugombeaji wa Ridhiwani ikiufananisha na undugunaizeisheni ambapo mambo hufanyika kwa kufuata mkondo wa undugu. Katika makala hiyo wanatajwa pia watoto wa vigogo walioajiriwa katika sehemu nyeti hapa nchini  katika kuushadidia undugunaizeisheni ambao mwandishi huyo anaufananisha na kitendo cha wana CCM wa Chalinze kumpigia kura za maoni Ridhiwani ili akawe mgombea wao.
Makala nyingine ilisema “Nateta na watoto wa marais wetu”. Hiyo inamsema Ridhiwani kwa staili tofauti, kwamba kwa nini akiwa mtoto wa rais anaonekana kutajwatajwa sana akihusishwa na mambo mbalimbali ukiwemo ukwasi wa kutisha unaosemekana anaumiliki katika umri wake mdogo, tofauti na watoto wa marais wengine waliomtangulia baba yake kwenye kiti hicho cha enzi. Lakini hata hivyo naye huyo anasema hayo yote kutokana na wana CCM wa Chalinze kumchagua Ridhiwani awe mgombea wao.
Kutokana na maneno hayo yanayosemwa dhidi ya kijana huyo, mtoto wa rais, namimi nimeona bora nichangie kidogo kujaribu kuweka mambo katika usawa wake, kusudi isijekuwa wivu, kinyongo, chuki nakadhalika, vinachukua nafasi ya kuwashawishi wananchi kwa njia ya upotoshaji vikionyesha kuwa ndivyo vilivyo sahihi.
Ridhiwani Kikwete ni mtoto wa rais, sawa, lakini vilevile ni raia kama walivyo raia wengine wote. Anayo haki ya uraia kama waliyo nayo wengine, kama mimi na wewe tulivyo. Sababu hakuna mahali popote palipoandikwa kwamba ukiwa mtoto wa rais haki zako nyingine za urai unazipoteza. Mpaka hapo sidhani kama ameishatoka nje ya mstari.
Undugunaizeisheni unaotajwa sielewi unaingiaje hapo. Kama pengine angetajwa tu kuwa sasa Ridhiwani Kikwete ndiye mbunge wa Chalinze pasipo kufuata taratibu za uchaguzi, hapo kweli hata mimi ningefikiria vingine. Lakini kagombea sawa na wengine, wanachama wamepiga kura za maoni na kumpendekeza kwa kishindo, sasa undugunaizeisheni unatoka wapi? Ina maana wanachama wote wa Chalinze  waliopiga kura za maoni ni jamii ya Kikwete?
Kitu kingine ni kwamba Ridhiwani ni kijana tena msomi, mwanasheria. Bilashaka atakuwa nayo matamanio ya ujana kama waliyo nayo vijana wengine. Ispokuwa yeye kama kijana msomi matamanio yake yatakuwa yanatofautiana na ya vijana ambao hawana kisomo kama alicho nacho yeye. Hivyo si kwamba kila kijana atatamani kuwa mbunge, la hasha, kila mmoja anapatamani anapopaweza. Hivyo Ridhiwani kuutamani ubunge ulio kwenye uwezo wake, kiusomi, kuna tatizo gani?
Ni pale tu kama angeutamani ubunge wakati tukielewa kuwa hauwezi, ambapo na mimi ningejiuliza maswali ya kwamba imekuwaje kitu kama hicho kikatokea. Na kama hali ingeendelea, mchakato wa ubunge, katika hali hiyo inayoonyesha kwamba ubunge hauwezi, basi undugunaizeisheni ungekuwa umejitokeza katika picha ya rangi.
Pamoja na Ridhiwani kuwa kijana msomi, mtoto wa rais, kizuri zaidi ni kwamba anajichanganya sana na watu bila kujali usomi wake wala utoto wa rais. Hana maringo yanayomfanya awabague watu kwa kufuata ni watu wa sampuli gani.
Na kawaida ya binadamu hupendelea kutumia kila nafasi inayopatikana kuwa karibu na wakubwa, kimazingira mtoto wa rais ni mtu mkubwa,  kwa vile anatoka katika familia ya kwanza katika nchi, familia  ambayo waingereza wanaita “first family”. Nafasi hiyo kwa Ridhiwani imewekwa wazi, kila anayetaka kuitumia ni ruksa ili awe karibu naye.
Kwahiyo inapotokea watu wakawa wanamsemasema sana sio kwamba wanamsema kwa ubaya, kama wengine wanavyotaka kupotosha, hapana, wanamsema kwa vile wanamuona, wanamuelewa, anajichanganya nao bila kuwabagua ilhali wakielewa kuwa sio mtu wa kada yao, yeye ni mtu kutoka kwenye familia ya kwanza hapa nchini. Je, watu kumsema kwa hilo la kujishusha chini na kuwa sawa na wao, linamfanyaje yeye aonekane ana makosa?
Ikumbukwe kwamba hiyo ni tofauti na watoto wengi wa marais wengine ambao watu walikuwa hawawaoni na kuwafahamu, pengine kutokana na watoto hao kutopenda kujichanganya na watu wakijiona wao ni matawi ya juu.
Kuhusu ukwasi unaosemekana Ridhiwani anao, sijui kuna ushahidi gani kuhusu hilo. Sababu karibu wote wanaosema Ridhiwani ana utajiri wa ajabu najua wanasemea hisia tu kwa vile hilo ni jambo gumu kulithibitisha.
Mfano, niliwahi kuwa mahala, mikoani, ndugu yangu mmoja akawa anakitaka kiwanja fulani kilichokuwa wazi pasipo na nyumba yoyote, tena katika eneo zuri. Ni moja ya viwanja vya manispaa vilivyokuwa vinagawiwa kwa ajili ya ujenzi wa kamazi ya watu.
Tulipokifuatilia mpaka makao makuu ya manispaa tukakuta kimeandikwa jina la Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kuwa ndiye anayekimiliki. Kwa waliokuwa hawamwelewi mtu huyo walijua kuwa kweli ndiye anayekimiliki, na kuna waliosema kwamba mtu huyo ni tajiri sana aliyejimilikisha viwanja kila kona ya nchi kwa kutumia cheo chake.
Kumbe mambo hayo yanafanywa na matapeli wanaofanya kazi kwenye manispaa. Wanatumia njia hizo za kuvipachika viwanja majina ya watu wakubwa kusudi viwanja hivyo visiguswe na hata vigogo wa mikoa, ambao katika hali ya kwaida ni vigumu kuwazuia kupata sehemu wanazozihitaji, ili baadaye wao hao matapeli waje waviuze kwa bei ya juu sana. Sioni jambo kama hilo haliwezi kufanyika kwa kutumia jina la Ridhiwani Kikwete linapokuja suala hilo  la ukwasi wake.
Kuhusu Ridhiwani kugombea ubunge, sioni tatizo lolote katika hilo. Hiyo ni haki yake ya kiraia. Pengine kama kuna wanaosema kwamba yeye sio raia wa nchi hii. Lakini kwamba yeye ni mtoto wa rais, hicho ni kichekesho. Maana kama nilivyosema awali, kuwa mtoto wa rais hakumvui mtu haki zake za kiraia.
Na kwamba baba yake alikuwa mbunge wa jimbo lilelile halafu akawa rais, ni hoja isiyo na mashiko sababu ikiangaliwa vingine itaonekana inajipinga yenyewe.
Mfano ni watoto wangapi ambao wazazi wao wote wawili, baba na mama, ni walimu au hata mmoja wao, halafu wakatokea watoto wao wawili na hata watatu, nao wakawa walimu? Je, kuna swali linaloulizwa kwa nini inakuwa hivyo?
Vivyohivyo kwa madaktari, wanasheria, polisi, wawindaji na hata wavuvi. Sababu mara nyingi kazi za wazazi huwa zinawatamanisha watoto kuzifuatilia kama watoto wanayo mapenzi ya dhati kwa wazazi wao. Ni mara chache sana watoto kukosa kufuata mkondo wa wazazi wao. Anayelishangaa hilo bora akapimwe akili zake kwanza.
Ndiyo maana tunaona watoto wengi ambao wazazi wao ni wanasiasa au walikuwa wanasiasa nao wanatamani kuwa wanasiasa.
Kwahiyo hili la Ridhiwani kamwe haliwezi kufananishwa na la watoto wa vigogo wanaoajiriwa kwenye sehemu nyeti za nchi. Kuajiriwa kunaweza kutokana na maelekezo, (….. muajirini mtoto wangu au mtoto wa fulani). Kamwe lugha ya aina hiyo haiwezi kutumika katika suala kama hili la Ridhiwani kugombea ubunge. Hakuna anayeweza kuwaamrisha wananchi wamchague mtoto wake awe mbunge wao. Kinachoamrisha ni mienendo ya Ridhiwani iliyokubaliwa na wapiga kura, basi.
Tena katika kulifuatilia hili nimegundua kuwa Ridhiwani kashawishiwa na kuombwa na wana Chalinze ili akachukue fomu na kugombea ubunge kwa ahadi kuwa watampa kura akawe mbunge wao. Sidhani kama baba yake anahusika katika hilo.
Kitu alichokuwa anaweza kukifanya baba yake, kilicho kwenye mamlaka tuliyomkabidhi kama rais, kilikuwa ni kumteua Ridhiwani awe mbunge na kisha amfanye kuwa waziri kama angetaka. Lakini hakufanya hivyo. Sasa wanaomsakama rais kwa mambo ambayo pengine hayaelewi wana maana gani?
Nitamshangaa sana Rais Kikwete, pale atakapokaa kama mwenyekiti wa CCM na kulifanya jina la mwanae liondolewe kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Chalinze, kama anavyoshauriwa na baadhi watu wanaomsakama bila hatia yoyote, wakati wananchi wa Chalinze wakiwa tayari wameishaonyesha nani wanamtaka awe mbunge wao. Kusema ukweli atakuwa hajawatendea haki.
Next Post Previous Post
Bukobawadau